Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeahirishwa tena baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha maombi ya kuendelea kuficha utambulisho wa baadhi ya mashahidi kwa sababu za kiusalama.
Kesi hiyo ilitajwa leo, Julai 15, 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo Lissu alionesha wazi kutoridhishwa na hatua hiyo, akidai kuwa upande wa Jamhuri unatumia hila kuchelewesha mchakato wa haki.
“Kwa mujibu wa sheria, hasa kifungu cha 262(6), taarifa ya kupeleka kesi Mahakama Kuu ingetakiwa kuwa imeshawasilishwa. Leo ni siku ya 97 nikiwa mahabusu pamoja na wafungwa waliokwishahukumiwa kunyongwa. Nimechoka na danadana hizi,” alisema Lissu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswaga.
Lissu ambaye anajiwakilisha mwenyewe, alipinga vikali maombi ya Jamhuri, akiitaka Mahakama kuliondoa shauri hilo kwa kuwa, kwa madai yake, upande wa mashtaka umeshindwa kutimiza wajibu wa kisheria na unamnyima haki.
Upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga, uliiambia Mahakama kuwa ushahidi wa shauri hilo umekamilika na kwamba ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imejiridhisha na uhalali wa mashitaka. Hata hivyo, wakaiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Mahakama Kuu itakaposikiliza na kutoa uamuzi juu ya maombi ya kuficha utambulisho wa mashahidi kwa sababu za kiusalama.
Katika utetezi wake, Lissu alisisitiza kuwa kesi hiyo ina sura ya kisiasa, ikizingatiwa kuwa imefunguliwa katika mwaka wa uchaguzi dhidi ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani. Alidai kuwa kesi hiyo imelenga kudhoofisha kampeni ya “No Reforms, No Election” inayoendeshwa na CHADEMA.
Baada ya kusikiliza hoja kutoka pande zote, Hakimu Franco Kiswaga alikubaliana na ombi la upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 30, 2025. Hata hivyo, aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha unakamilisha taratibu husika kwa haraka ili mshtakiwa apate haki yake kwa wakati.