Kigogo TPA atumbuliwa

Rais Samia Suluhu Hassan leo tarehe 4 Julai, 2022 ametengua uteuzi wa mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Eric Hamisi na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa naibu wake, Plasduce Mkeli Mbossa. 

Rais Samia amechukua uamuzi huo saa chache baada kusema haridhishwi na kasi ya utendaji wa bandari za Tanzania na kuwataka watendaji waache siasa na longolongo wakati wa utekelezaji majukumu yao.

Awali akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), iliyofanyika mapema asubuhi leo ikulu  jijini Dar es Salaam, amesema Bandari ya Dar es Salaam, ingekuwa inafanya kazi vizuri, mapato yake yangegharamia nusu ya bajeti ya Serikali kila mwaka.

“Siridhishwi kabisa na kasi za bandari, siasa na longolongo zilizopo, huko nje mabandari yanaendeshwa kwa kasi kubwa, yanaendeshwa kwa operesheni na biashara zinaenda kwa kasi zaidi. Mwekezaji anakuja ni kuzungushwa mwanzo mwisho. Bandari wafanye kazi tutatupia jicho vizuri kwenye masuala ya bandari wale waliokabidhiwa bandari nataka tuelewane vizuri.

“Bandari hii ikifanya kazi vizuri nusu ya bajeti tunayopanga kila mwaka, itatolewa bandari ya Dar es Salaam, lakini tu kama tutajipanga tufanye kazi vizuri kama bado tunakwenda kwa longolongo hilo lengo hatutafikia, nawaomba wajiange vizuri tujenge kwa kasi,” amesema Rais Samia.

Eric Hamisi ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo tarehe 4 Aprili mwaka jana, kabla ya uteuzi huo alikuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania.

Hamisi alichukua nafasi ya Mhandisi Deusdedit Kakoko aliyetumbuliwa na Rais Samia tarehe 28 Machi mwaka huu, kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa shilingi bilioni 3.6 bandarini ambapo aliagiza Takukuru kufanya uchunguzi.

Rais Samia alitoa maagizo hayo baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali nchini- CAG, Charles Kichele, pamoja na ya taasisi ya kupambana na rushwa TAKUKURU ya mwaka 2019 na 2020.