Kikosi kazi chapendekeza mchakato wa Katiba Mpya Tanzania uanze baada ya uchaguzi 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Kikosi Kazi cha kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Prof Rwekaza Mukandala Ikulu Jijini Dar leo

Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa na uendeshaji wa uchaguzi nchini Tanzania, kilichoteuliwa na msajili wa vyama vya siasa nchini humo, Jaji Francis Mutungi kimependekeza mchakato wa kupata Katiba Mpya uanze baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akikiagiza kulifanyia kazi na kupeleka mapendekezo.

Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, kinachojumuisha wajumbe 25 kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo wanasiasa, asasi za kiraia, wanazuoni na wadau wa kamati za ulinzi na usalama Profesa Rwekaza Mukandara ametoa mapendekezo hayo wakati akiwasilisha taarifa ya awali ya utendaji kazi wa kikosi hicho, kwa Rais Samia, Ikulu jijini Dar es salaam.

Kazi kubwa ya kikosi kazi hicho ni kuangalia na kuchambua mwenendo wa hali ya demokrasia na namna ya kutatua changamoto zinazoikumba baadhi ya vyama vya siasa, ikiwemo mikutano ya hadhara.

Katika maelezo yake, Profesa Mukandara amesema sababu za kutoa pendekezo hilo ni pamoja na kutoa fursa ya kuanisha dira mpya ya maendeleo ya miaka ijayo, itakayotoa mwelekeo wa Katiba mpya.

“Pia kuna suala la kukosekana kwa muda wa kutosha kuanza kutumia Katiba mpya ndani ya kalenda ya uchaguzi 2025. Kuna haja ya kutoa fursa ya kufanya marekebisho ya sheria ya uchaguzi na kanuni zake.”- Amesema na kuongeza kuwa

“Jambo jingine ni kuna haja ya kutoa fursa ya kutosha ya kufanyia kazi masuala ya muda wa kati ikiwa ni pamoja na kuanisha masuala ya dira ya maendeleo,” amesema Profesa Mukandara.

Mara baada ya wasilisho la taarifa hiyo, Rais Samia amewaambia kikosi hico kuwa wakafanyie kazi suala hilo, kwa kufanyia kazi marekebisho ili kuona kama kuna haja ya na sio kuandika katiba mpaya.

 “Hili la Katiba mpya mtakwenda kulifanyia kazi na mtaleta mapendekezo yatakayotangazwa Watanzania wote wayaelewe, Mimi nakubaliana kuwa ni jambo la muda mrefu lakini Watanzania wote waelewe, amesema Rais Samia na kuongeza” 

“Lakini kwanza tukayafanyie kazi haya marekebisho tuliyoyasema haya kipindi hichi cha muda wa kati halafu huko mbele tuone je tuna haja ya kurekebisha katiba yetu pengine kutakuwa na haja sio ya kuandika mpya, kurekebisha baadhi ya maeneo na hata kama tunaandika mpya lakini kazi kubwa inakuwa imefanyika kwenye marekebisho ambayo tunakuwa tumeyafanya kule ni kwenda kuingiza tuu kwenye hiyo katiba.”  Amesema Rais Samia.

Nchini Tanzania kumekuwa na vuguvugu la madai ya Katiba Mpya, kwa madai kuwa katika iliyopo sasa ina mapungufu ya kisheria na inatoa nguvu kubwa kwa kiongozi aliyopo madarakani.

Hata hivyo pamoja na madai hayo Serikali iliyopo mamlakani imesema suala la Katiba mpya sio kipaumbele kwa sasa na kwamba suala hilo litasubiri.