Kikwete amjibu Polepole kuhusu utaratibu wa CCM: “Hakuna jambo jipya, utaratibu umeheshimiwa”

Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete amejibu hadharani hoja zilizotolewa na kada wa Chama cha Mapinduzi Humphrey Polepole kuhusu madai ya ukiukwaji wa taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kugombea urais kwa muhula wa pili.

Akizungumza katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, Kikwete alisema utaratibu wa chama hicho ni wa wazi na umekuwa ukiheshimiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

“Najua kulikuwepo na maneno au vijineno eti utaratibu umekiukwa na mimi nililaumiwa kwa jinsi nilivyosema pale kwenye mkutano mkuu, lakini nasema waliokuwa wanasema hayo ama hawafahamu utaratibu wa chama chetu na kama wanafahamu labda wamesahau au wanajifanya hamnazo,” alisema Kikwete.

Kwa mujibu wa Kikwete, utaratibu wa chama umekuwa ukimhakikishia Rais aliye madarakani nafasi ya pekee kugombea kipindi cha pili iwapo atakuwa na nia ya kuendelea. Alitolea mfano marais waliomtangulia na kumfuata ambao ni Rais Benjamin Mkapa (1995–2005) alipewa nafasi hiyo mwaka 2000, Rais Jakaya Kikwete (2005–2015) aliwekewa utaratibu huo mwaka 2010 na Rais John Magufuli (2015–2021) naye hakupingwa ndani ya chama alipogombea muhula wa pili mwaka 2020.

 

“Kwa nini leo kuwe na kelele za kutaka tofauti kwa Rais Samia, sababu yake nini? Mbona haya hatujayasikia kwa Mkapa, hatujayasikia kwa Kikwete na wala hatujasikia kwa Magufuli,” aliongeza Kikwete huku akishangaa madai hayo kuibuliwa na watu waliokuwapo katika mchakato wa awali.

Polepole na madai ya ukiukwaji

Siku kadhaa zilizopita, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba Humphrey Polepole, ambaye pia ni mwanachama wa CCM na Mbunge wa zamani, aliibua hoja kwamba utaratibu wa chama juu ya uteuzi wa mgombea urais haukufuatwa ipasavyo safari hii. Polepole alidai kuwa kulikuwa na “kuharakishwa” kwa mchakato wa ndani na kutotolewa nafasi pana kwa wanachama kujadili mustakabali wa chama na nchi.

Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa ndani na nje ya chama, hasa ikizingatiwa kwamba CCM ndiyo chama kinachoshikilia dola tangu uhuru. Polepole alisisitiza kuwa hoja yake si kupinga uongozi wa Rais Samia, bali ni kutaka chama kishikamane kwa kufuata katiba na kanuni zake.

Kikwete: “Samia ameridhisha, ndiyo maana amepewa ridhaa”

Katika hotuba yake, Kikwete alisema kilichoibua mwangwi wa “Samia miaka mitano tena” si kupuuzwa kwa taratibu, bali ni kuridhika kwa wana-CCM na Watanzania kwa kazi alizozifanya Rais Samia tangu achukue madaraka Machi 19, 2021.

“Ni mara ya kwanza nchi kukumbwa na changamoto kubwa ya kumpoteza Rais akiwa madarakani. Lakini Samia alichukua uongozi katika mazingira magumu na akaonyesha uthabiti. Ndiyo maana leo wapo wanaosema aendelee muhula mwingine,” alisema Kikwete.

Kauli za viongozi hao wawili zinakuja katika wakati ambapo Tanzania ipo katika mchakamchaka wa Uchaguzi Mkuu ambapo si Polepole pekee ambaye ameibua hoja za kutoridhishwa na mchakato wa uteuzi wa kiongozi ndani ya CCM bali hata baadhi ya WanaCCM wamekuwa na maoni tofauti juu ya mchakato huo ikiwemo wengine kuhama chama.