Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Tanzania imekamata kilo 16.643 za dawa za kulevya zikiwamo kilo 15.19 za heroin.
Dawa hizo aina ya heroin zimekamatwa kwa watuhumiwa watatu ambao ni washirika wa Kambi Seif na wenzake waliokamatwa mwanzoni mwa Novemba wakiwa na kilo 34.89 za heroin.
Kiwango hicho kinafanya jumla ya dawa za kulevya zilizokamatwa kwa Kambi na washirika wake kufikia kilo 50.08.
Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Gerald Kusaya amewataja watuhimiwa hao ni Suleiman Ngulangwa (36), Sharifa Bakar (41) na Farid Said (22) wote wakazi wa Dar es Salaam.
Watuhumiwa wengine wanne walikamatwa na gramu 655.75 za cocaine na gramu 968.67 za metamphetamine, kulingana na Kusaya hawa walikamatwa wakiwa kwenye harakati za kusafirisha dawa hizo.
Waliokamatwa katika operesheni hiyo ni Irene Mseleku (39) mkazi wa Shinyanga, Hussein Mtitu (28), Jaalina Chuma (31) na Shaban Said (36) wote wakazi wa Dar es Salaam.
“Kutokana na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya nchini, wahalifu wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali ili kufanikisha uhalifu wao. Hata hivyo mamlaka iko macho na tunaendelea kukabiliana na mbinu hizo.
“Tunashirikina na kampuni za usafirishaji wa vifurushi, vyombo vya ulinzi na usalama na wadau wengine katika kudhibiti ili kukabiliana na mbinu mpya za usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya,” amesema Kusaya.
Katika hatua nyingine Kusaya amewaonya wasanii wanaotunga nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya na kueleza kuwa hatua zitachukuliwa dhidi yao endapo itathibitika wanafanya hivyo.