Mamlaka nchini Malawi zinasema idadi ya watu ambao bado hawajulikani walipo kufuatia Kimbunga Freddy imeongezeka kutoka 349 hadi 427, huku nchi nyingi zikiendelea kutuma misaada ya kibinadamu.
Idara ya Masuala ya Kukabiliana na Majanga ya Malawi (DoDMA) siku ya Jumatatu ilisema ilipokea ripoti za tathmini ya haraka kutoka mikoa 15 iliyoathirika nchini humo.
“Kufikia Jumatatu, Machi 20, 2023, idadi ya watu waliokimbia makazi yao ni 508,244.
Idadi ya vifo imeongezeka kutoka 476 hadi 499, na majeruhi 1,332,” DoDMA ilisema katika taarifa. Nchi kadhaa zikiwemo Uingereza, Tanzania na Zambia zimetuma timu kusaidia katika shughuli za uokoaji.
Dhoruba hiyo ilipiga Msumbiji na Malawi wiki jana kwa mara ya pili ndani ya mwezi mmoja, na kuharibu nyumba nyingi na kusababisha mafuriko makubwa.
Serikali ya Malawi imeweka kambi zaidi ya 500 katika eneo la kusini mwa nchi hiyo, ambapo hadi wilaya 10 zimeathirika.