KINA MBOWE WAWEKA PINGAMIZI LINGINE TENA

Jopo la mawakili wa utetezi katika kesi inayomkabili mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu wamepinga hati ya kukamatia mali iliyowasilishwa na Shahidi wa 8, kwa kile walichodai kuwa hati hiyo imeandaliwa kwa sheria ambayo haipo nchini Tanzania. Pingamizi hilo limekuja wakati ambapo shahidi huyo wa upande Serikali akiwa anatoa ushahidi wake mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

SP Jumanne Malangahe ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wakati akiongozwa na wakili wa Serikali Robert Kidando aliiomba mahakama ichukue nyaraka hiyo kama kielelezo cha ushahidi wake mahakamani hapo. Hata hivyo upande wa utetezi ulipinga ombi hilo, hali iliyoibua hoja za kisheria kutoka pande zote mbili ambapo mbishano wa hoja hizo ulichukua takribani zaidi ya saa moja mahakamani hapo.

Wakili wa Utetezi Nashon Nkungu ameiambia mahakama kwamba hati hiyo imeletwa mahakamani chini ya kifungu cha 38 (3), cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai iliyofanyiwa marekebisho 2018, wakati sheria hiyo haipo. Hoja ya wakili Nashon imeungwa mkono na mawakili wote wa utetezi ambapo kwa upande wa wakili Peter Kibatala ameiomba mahakama hiyo isiipokee hati hiyo akidai haina uhai wa kisheria mahakamani hapo sababu hakuna sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai iliyorekebishwa 2018, bali iliyopo ilirekebishwa 2019. Hivyo, mawakili wa jamhuri walipaswa kuieleza mahakama kulikuwa na makosa ya uchapaji.

Wakati mawakili wa utetezi wakisema hayo mawakili wa Serikali wakiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali Robert Kidando wameiomba mahakama kwamba itupilie mbali hoja zilizotolewa na utetezi kwenye pingamizi hilo wakisema hoja zao hazina mashiko. Ni takribani zaidi ya mapingamizi matatu kutolewa na jopo la mawakili wa upande wa utetezi tangu kuanza kwa kesi hii.
 

Mapema leo asubuhi kwenye ushahidi wake ASP Jumanne aliieleza mahakama namna alivyowapekua watuhumiwa Adam Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Ling’wenya, mnamo tarehe 5 Agosti 2020, baada ya kuwakamata maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Malangahe amedai kuwa Agosti 4, 2020 akiwa kwenye kituo chake cha kazi huko Arumeru majira ya jioni alipokea simu kutoka kwa Afande Ramadhani Kingai iliyotaka ajiandae muda wowote kuwa anatakiwa kwenda kwenye kazi mkoani Kilimanjaro mjini Moshi. Malangahe amesema mara baada ya simu hiyo muda mchache baadae alimuona Kingai akiwasili ofisini kwake akiongozana na askari wengine akiwemo afande Mahita, Koplo Francis, Afande Godluck na Afande Azizi Amedai kuwa Kingai alimwambia kuwa kuna taarifa za uwepo wa kikundi cha wahalifu ambacho kilikua kinatarajia kufanya matukio ya uhalifu hapa nchini kwa kulipua vituo vya mafuta, kuanzisha vurugu, kufanya maandamano, kukata miti au magogo kwenye barabara ili kuzuia magari kupita pamoja na kuwadhuru viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya.

Malangahe ameileza mahakama kuwa maelezo ya Kingai yalikua ni kwamba kundi hilo la uhalifu linaratibiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe huku miongoni mwa wahalifu hao watatu kati yao walishawasili Moshi.Baada ya kupokea maelezo hayo kutoka kwa afande Afande Kingai majira ya saa moja usiku walianza safari kutoka ofisini kwake Arumeru kuelekea Moshi ambapo huko walifika majira ya usiku wa saa 2.

Asubuhi ya Agosti 5, 2020, wakiwa Moshi walipata taarifa kwamba watuhumiwa wapo eneo la Rau Madukani na watuhumiwa hao walikua watatu kama walivyoelekezwa mmoja alikua amevaa jezi ya Taifa Stars wawili walikua wamevaa mashati ya mikono mirefu. Baada ya kupata taarifa hizo walikwenda maeneo husika ambayo watuhumiwa walikuwepo na walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Ling’wenya na Kasekwa huku mtuhumiwa wa tatu wasijue amekimbilia wapi.

Kwa mujibu wa ASP Jumanne, washtakiwa hao baada ya kupekuliwa, mmoja ambaye ni Kasekwa, alikutwa na simu, silaha aina ya bastola yenye silio namba A5340 ambayo ina risasi tatu na kete 58 ambazo baadae ziligundulika kuwa ni za dawa za kulevya. Huku mwenzake Ling’wenya alidaiwa kukutwa na kete 25 za dawa hizo pamoja na simu aina ya Smartphone.

Kufuatia pingamizi lililowekwa na upande wa utetezi Jaji Joachim Tiganga aliahirisha kesi. Freeman Mbowe na wenzake wanakabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi yenye makosa ya ugaidi ndani yake ambapo katika kesi hiyo Mbowe anadaiwa kuwa kinara wa mipango ya kutaka kutenda vitendo vya ugaidi kwa kulipua vituo vya mafuta, kukata miti katika sehemu mbalimbali nchini pamoja na kutaka kuwadhuru viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya.