Mahakama nchini Ivory Coast siku ya Jumanne ilimwondoa rasmi kiongozi mkuu wa upinzani, Tidjane Thiam, katika orodha ya wapiga kura, na hivyo kumzuia kushiriki katika uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Thiam, ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa kiongozi wa chama cha Democratic Party of Ivory Coast (PDCI), ameondolewa kwa madai kuwa alipoteza uraia wa Ivory Coast baada ya kupata uraia wa Ufaransa mwaka 1987.
Uamuzi huo umetajwa na Thiam kuwa “kitendo cha kuharibu misingi ya demokrasia.” Taarifa kutoka kwa wakili wake, Ange Rodrigue Dadje, zinasema kuwa mahakama ilikubali hoja kwamba Thiam alipoteza uraia wake wa Ivory Coast alipokubali kuwa raia wa Ufaransa, hivyo akafutwa katika orodha ya wapiga kura.
Mawakili wa Thiam wamesema kesi hiyo ni ya kisiasa na inalenga kumzuia kugombea urais. Uamuzi huo hauwezi kukatiwa rufaa. Maswali kuhusu uraia wake yamekuwa yakimkabili tangu alipotangaza nia ya kugombea.
Ingawa Thiam alizaliwa Ivory Coast na kupewa uraia wa Ufaransa mwaka 1987, aliuacha uraia huo mwezi Machi ili aweze kugombea kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo ambazo haziruhusu wagombea wenye uraia pacha.
Hata hivyo, maadui wake wa kisiasa walitumia kifungu cha 48 cha sheria ya uraia ya miaka ya 1960, ambacho kinasema kuwa mtu anayepata uraia mwingine hupoteza uraia wa Ivory Coast.
Bernard N’zi Kokora, aliyewasilisha kesi hiyo, alisema, “Ilikuwa ni wajibu wangu kama raia kuheshimu sheria na naamini mahakama imetenda haki.”
Thiam na wafuasi wake wamekuwa wakilalamikia kile wanachokiita ni mbinu za serikali kudhibiti uchaguzi kwa kuiondoa PDCI katika kinyang’anyiro. “Uamuzi huu ni kitendo cha uharibifu wa kidemokrasia na unawaengua mamilioni ya wapiga kura,” alisema Thiam katika taarifa yake.
Simon Doho, kiongozi wa wabunge wa PDCI, alisema, “Tumeingia kwenye siasa na tumeacha haki. Hii ilikuwa kesi ya kisiasa.”
Msemaji wa chama tawala cha RHDP, Mamadou Toure, alisema, “Tunapohukumiwa kwa faida yao, mahakama ni huru, lakini ikihukumu kinyume, inatajwa kuwa imetumika. Hatuna cha kusema kuhusu uamuzi huu wa mahakama.”
Chama cha PDCI kilimteua rasmi Thiam kuwa mgombea wake siku ya Alhamisi iliyopita. “Oktoba 2025 bado ni mbali, lakini najua sitaachwa salama,” alisema Thiam.
Wagombea wengine mashuhuri pia wameondolewa katika kinyang’anyiro, akiwemo rais wa zamani Laurent Gbagbo, mshirika wake wa karibu Charles Blé Goudé, na waziri mkuu wa zamani aliye uhamishoni Guillaume Soro, wote kwa misingi ya maamuzi ya mahakama.
Chama tawala bado hakijamtangaza rasmi mgombea wake, lakini kimetoa wito kwa Rais Alassane Ouattara mwenye umri wa miaka 83, ambaye amekuwa madarakani tangu 2011, kugombea muhula wa nne. Mkutano wa chama hicho utafanyika mwezi Juni.