Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kimetangaza kuwa mmoja wa viongozi wake amekamatwa Jumatatu usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati akijiandaa kusafiri kwenda Ubelgiji kushiriki mkutano wa kidemokrasia.
Tukio hilo ni miongoni mwa matukio kadhaa ya hivi karibuni yanayowalenga wanachama wa CHADEMA, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.
Kwa mujibu wa msemaji wa chama hicho, Brenda Rupia, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Amani Golugwa, alikamatwa saa 6:45 usiku na anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.
“Golugwa sasa yuko Kituo Kikuu cha Polisi,” alisema Rupia.
Golugwa alikuwa akisafiri kuelekea Brussels, Ubelgiji, kuiwakilisha CHADEMA katika mkutano wa International Democracy Union (IDU) — jukwaa la kimataifa la vyama vya siasa vya mrengo wa kati-kulia.
Katika taarifa yao, polisi wa Dar es Salaam walithibitisha kumkamata Golugwa, wakisema kuwa walipokea taarifa za kiintelijensia kwamba alikuwa akiondoka na kurejea nchini kinyume cha sheria. Uchunguzi zaidi unaendelea.
Hata hivyo, IDU ililaani vikali tukio hilo kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), wakilitaja kuwa ni “kukamatwa kinyume cha sheria” na kutaka Golugwa aachiwe mara moja.
“Kunyoosha mkono wa chuma dhidi ya sauti za upinzani ni kuvunja misingi ya demokrasia,” ilisema IDU katika taarifa yao.
Kabla ya kukamatwa, Golugwa alizungumza Jumamosi kuhusu kutoweka kwa mmoja wa wafuasi wa CHADEMA, ambaye inadaiwa alitekwa na watu waliotambulika kuwa maafisa wa polisi. Licha ya polisi kuahidi uchunguzi, bado hakuna taarifa yoyote kuhusu alipo.Golugwa alitoa muda wa saa 72 kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi kutoa maelezo juu ya tukio hilo na mengine ya watu kutoweka kwa mazingira ya kutatanisha.
Mapema mwaka huu, CHADEMA ilitangaza kuwa haitashiriki uchaguzi wowote usioambatana na mageuzi ya kweli, yakiwemo kuwa na tume huru ya uchaguzi, na miongozo wazi inayozuia wagombea wake kuondolewa katika kinyang’anyiro.
Hivi karibuni, chama hicho kiliondolewa rasmi kushiriki uchaguzi kwa kukataa kusaini “kanuni za mwenendo wa uchaguzi”.