Kiongozi wa upinzani Uganda ajificha, mwingine akiwa mahututi hospitalini

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema yuko mafichoni kufuatia uchaguzi wa wiki iliyopita, huku kiongozi mwingine wa upinzani, Kizza Besigye, akiwa mahututi kutokana na hali mbaya ya afya, kwa mujibu wa mke wake.

Akizungumza na shirika la habari la AFP siku ya Jumatano, Bobi Wine alisema analazimika kujificha baada ya uchaguzi wa Januari 15, 2025, uliomrejesha madarakani Rais Yoweri Museveni kwa muhula wa saba. Wine ameitaja matokeo ya uchaguzi huo kuwa ni “wizi wa wazi”.

Rais Museveni mwenye umri wa miaka 81, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, anatuhumiwa kudhibiti kwa karibu mifumo ya uchaguzi na usalama nchini humo.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, Museveni alipata asilimia 71.65 ya kura, ikilinganishwa na asilimia 24.72 za Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, mwanamuziki wa zamani wa ragga aliyebadili mwelekeo na kuingia kwenye siasa akiwa na umri wa miaka 43.

Waangalizi wa uchaguzi na mashirika ya kiraia (NGOs) wamekosoa vikali matokeo hayo, wakieleza kuwepo kwa kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kwa siku kadhaa pamoja na ukandamizaji wa wapinzani.

 

-Vitisho vya Kifo-

Bobi Wine, ambaye aliwahi kukamatwa na kuteswa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2021, alishiriki katika uchaguzi wa mwezi huu lakini alilazimika kuingia mafichoni baada ya vikosi vya usalama kuvamia nyumbani kwake.

“Niko sawa, niko salama, lakini kwa sasa niko mafichoni. Familia yangu, mke wangu na jamaa zangu wamekuwa chini ya kifungo cha nyumbani kwa wiki moja,” alisema Wine alipoongea na AFP kwa simu.

Ameongeza kuwa amekuwa akihama hama, lakini analindwa na kuhifadhiwa na wananchi wa kawaida, hasa watu wa mitaa ya mabanda.

Rais Museveni pamoja na mwanawe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, wamekuwa wakiwatuhumu viongozi wa upinzani kuwa ni “magaidi”.

Siku ya Jumanne, Kainerugaba mwenye umri wa miaka 51, ambaye ameonyesha wazi nia ya kumrithi baba yake, alitishia kupitia mtandao wa X kumtafuta na kumuua Bobi Wine.

“Mimi si mhalifu wala gaidi. Mimi ni mgombea urais, na si kosa kugombea dhidi ya baba yake,” alisema Wine.

Aliongeza kuwa ni kosa kubwa kwa jeshi kuingilia uchaguzi, kuua watu na kuhatarisha maisha ya viongozi wa kisiasa.

 

Besigye Akiwa Mahututi Gerezani

Kiongozi mwingine mashuhuri wa upinzani, Kizza Besigye, ambaye ni daktari binafsi wa zamani wa Rais Museveni na mpinzani wake wa kisiasa kwa zaidi ya miaka 25, hakuweza kushiriki katika uchaguzi huo.

Besigye alitekwa nyara mwezi Novemba 2024 alipokuwa safarini nchini Kenya, kabla ya kurejeshwa Uganda ambako amekuwa akinyimwa dhamana akisubiri kesi yake.

Mke wake, Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la UNAIDS, alisema kuna njama ya kumuua mume wake akiwa gerezani.

Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa X siku ya Jumatano, Byanyima alisema Rais Museveni “anataka Besigye afe akiwa gerezani” na kudai ahamishiwe hospitali ya kawaida ili apatiwe matibabu na daktari wake binafsi.

Byanyima alisema aliruhusiwa kumtembelea mume wake na kumkuta akiwa amekaa kwenye kiti cha plastiki kichafu, akiwa dhaifu kupita kiasi, hali aliyosema inaashiria kuwa maisha yake yako hatarini.

 

Zaidi ya Watu 600 Wakamatwa

Besigye alipangwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatano, lakini wakili wake, Erias Lukwago, aliiambia AFP kuwa mfungwa huyo hakuweza kufikishwa mahakamani kutokana na hali yake ya afya.

Makundi ya kutetea haki za binadamu na upinzani wa Uganda yanasema kutekwa na kushtakiwa kwa Besigye kunahusiana moja kwa moja na uchaguzi wa hivi karibuni.

Lukwago amesema zaidi ya watu 600 wamekamatwa baada ya uchaguzi huo kwa tuhuma za kupinga ushindi wa Rais Museveni.

Siku chache kabla ya kupiga kura, Umoja wa Mataifa ulionya kuwa uchaguzi huo ulikuwa unafanyika katika mazingira ya “ukandamizaji na vitisho vilivyoenea”.

Akizungumzia mustakabali wake na wa chama chake, Bobi Wine alisema hana mpango maalum.

“Katika utawala wa kidikteta, hupangi mikakati bali unajibu ukandamizaji unaojitokeza,” alisema.

“Uganda inapigania demokrasia yake. Tunauomba ulimwengu uungane nasi, msituache peke yetu, msituache.”