Kishikwambi kingine cha sensa chaibiwa Moshi

Msimamizi wa Maudhui katika Sensa ya Watu na Makazi Kata ya Rau, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ameibiwa kishikwambi baada ya kuacha begi dukani kwa mtu.

Mratibu wa Sensa Mkoa wa Kilimanjaro, Albert Kulwa ametoa taarifa hiyo leo Ijumaa Agosti 26, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, ambapo amesema tukio hilo ni la kizembe na limetokea Agosti 25.

Kwa mujibu wa Kulwa, msimamizi huyo alipomaliza majukumu yake jioni alikwenda katika duka lililopo jirani na kuomba ahifadhiwe begi lakini ghafla begi hilo likapotea kwenye mazingira ya kutatanisha.

“Kimeibiwa kishikwambi kimoja, ambapo ameibiwa msimamizi wa maudhui, na ni uzembe maana alikwenda kwenye duka akamuomba mwenye duka ambaye ni dada amshikie begi akaenda kusambaza fomu,” amesema Kulwa.

 “Baada ya kuhojiwa wanasema alikuja kijana mmoja akawa anamsemesha kama kumzuga, dada akaingia ndani na aliporudi hakukuta begi hilo, unaweza kuanza kupata picha hapa ni uzembe.”

Aidha amesema msimamizi huyo na muuza duka wanashikiliwa Kituo cha Polisi Majengo kwa ajili ya mahojiano na kwamba wanaamini Jeshi la Polisi liko makini na kishikwambi hicho kitapatikana.

Amesema tayari wametoa maelekezo kwa makarani na wasimamizi kutunza vifaa walivyopewa ikiwemo vishikwambi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa makini muda wote ili kuepuka kuibiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa linamshikilia msimamizi huyo kutokana na kupotea kwa  kishikwambi hicho.

Kamanda  amesema uchunguzi unaendelea  ili kujiridhisha kama ndani yake kulikuwa  na nia ovu na kueleza kuwa haiwezekani ubebe begi ambalo unajua ndani yake lina kifaa muhimu halafu unaenda dukani na kuomba uhifadhiwe lakini ghafla linaibiwa.

“Sisi polisi tunaendelea na upelelezi wetu ili kujiridhisha kama ni upotevu wa njia ya kawaida ama ndani yake kulikuwa na njama za kupoteza kishikwambi hicho na upelelezi wa awali inaonyesha ni uzembe na sio wizi kama ambavyo watu wanataka kuamini,”amesema.

Akizungumzia kasi ya Sensa kwa Mkoa huo, Mratibu Kulwa amesema kasi itaongezeka katika kipindi  cha mwishoni kwa kuwa wasimamizi watageuka makarani na  kuingia mtaani kukusanya taarifa.

“Tumejipanga kwa siku hizi zilizobaki, kasi itaongezeka, wale wasimamizi watageuka kuwa makarani katika dakika za mwisho kwa sababu nao wamefundishwa, ili kuhakikisha tunamaliza kazi hii ndani ya muda uliopangwa.”