Mbunge wa Viti Maalum Jesca Kishoa amesema kauli za baadhi ya watu wakiwemo wanasisa wanaosema wakazi wa Ngorongoro mkoani Arusha wasihamishwe kwani wamezoea eneo hilo ni kauli za kuwagawa watanzania.
Mbunge huyo ambaye ni miongoni mwa wabunge 19 waliofukuzwa uanachama wa CHADEMA, ameyasema hayo jana wakati akichangia mjadala wa Bajeti 2022/23.
Amesema kauli hizo zinaweza kujenga matabaka na kufanya wananchi kwenye maeneo mengine nao kugoma kuhama kupisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Amefafanua wanaosema wananchi wa Ngorongoro kuwahamisha eneo lile ni makosa kwa sababu wameshayazoea, huko ni kutengeneza ‘Double standard’ ya hali ya juu katika taifa la Tanzania kwasababu kama hilo likisikilizwa maeneo mengine wakihamishwa kupisha miradi ya maendeleo watakataa.
“Kuna baadhi ya watu wanaopotosha kuhusu mchakato huu wa kuwahamisha baadhi ya wakazi wa Ngorongoro mkoani Arusha na miongoni mwa wanaopotosha wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamegeuza mchakato huo kama sehemu ya kutafuta kiki badala ya kuangalia maslahi mapana ya nchi,”amesema Mbunge Kishoa.
Amesisitiza kuna baadhi ya watu wanaaminishwa eneo hilo kuna Mwarabu anataka kulichukua na hizo ni propaganda za hovyo zinazofanywa na watu wanatafuta kiki.
”Kuna baadhi ya wanasiasa wanatafuta kiki, ukweli binafsi ninapowasikia najisia vibaya, nipo kwenye nchi ambayo kuna mwananchi yupo nchi nyingine lakini kazi yake ni kumtukana Rais wa Tanzania.Hili jambo sio nzuri kabisa na hakuna anayeweza kulivumia.”
Akizungumzia mchakato wa kuhamishwa kwa hiyari wakazi wa eneo hilo kwenda wilayani Handeni mkoani Tanga, Mbunge Kishoa anasema anatamani naye angekuwa miongoni mwa wanaohamishwa Ngorongoro kwani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imewatendea haki kwa kuwapa huduma zote za msingi na bora ambazo mwananchi yoyote anatakiwa kuzipata.
“Unapewa hati kama una wake watatu unapewa hati ya nyumba tatu,kwa upendo huu mkubwa wa Serikali kwa wananchi wa Ngorongoro nami naomba leo hii nitangaze rasmi kuanzia sasa naitwa Ole Kishoa ili nipelekwe kule nikapewe nyumba ya bure kabisa,”
Aidha amesema wanansiasa na wanaharakati wanapaswa kuacha kutumia kiraka cha Haki za Binadamua kwenye suala la mgogoro wa Loliondo na Ngorongoro linaloendelea nchini Tanzania.
Amesema ana taarifa kwamba kuna baadhi ya wabunge wanatetea kwa maslahi yao binafsi kwa kuwa wana mashemeji zao maeneo hayo.