Baraza la Mawaziri nchini Uganda limeidhinisha kupitishwa kwa Kiswahili kama lugha rasmi nchini humo.
Baraza hilo pia lilipendekeza ufundishaji wa Kiswahili katika shule za msingi na sekondari uwe wa lazima.
Kiswahili, ambacho asili yake ni Afrika Mashariki, ni mojawapo ya lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani ikiwa na wazungumzaji takriban milioni 200.
Lugha na lahaja zake huzungumzwa kutoka sehemu za Somalia hadi Msumbiji na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Twitter, baraza la mawaziri la Uganda lilisema uamuzi huo umefuatia agizo la Jumuiya ya Afrika Mashariki la kupitisha lugha hiyo ili kurahisisha mawasiliano kati ya nchi wanachama.
Itakumbukwa kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO tarehe 23 mwezi Novemba mwaka 2021 lilitangaza rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.
Maudhui ya maadhimisho ya mwaka huu ni Kiswahili kwa amani na ustawi. Lengo hasa la maadhimisho haya ya mwaka ni kusongesha matumizi ya lugha ya kiswahili kama nguzo ya amani, na ustawi na wakati huo kuimarisha tamaduni mbalimbali.
UNESCO ilipitisha uamuzi huo huko makao makuu yake mjini Paris Ufaransa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika hilo.
Azimio lilipitishwa bila kupingwa na utekelezaji wake unaanza mwaka huu wa 2022.