Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi (53) na mwenzake wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaama kwa kosa la kujifanya maofisa usalama huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.
Akisoma hati ya mashtaka katika mahakama hiyo Januari 27, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwanaamina Kombakono mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngimilanga, alidai katika shitaka la kwanza lililofanyika Desemba 24, 2021 katika ofisi ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT), mshtakiwa Muabi kwa nia ovu alijitambulisha kama ofisa usalama wakati akijua si kweli.
Katika shitaka la pili inadaiwa kwamba Julai 10, 2021 katika ofisi hizo za BOT washitakiwa wote Kwa pamoja walijitambulisha kwa Clay Apio kuwa wao ni maofisa usalama wakati wakijua si kweli.
Mbali na Muabhi mwingine ni mfanyabiashara Yusuph Yusuph (33) ambao kwa pamoja walitenda makosa hayo Katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam
Hata hivyo, washitakiwa hao wamekana kutenda makosa hayo, lakini upande wa mashitaka umesema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika
Baada ya maelezo hayo Hakimu, Ngimilanga alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wakiwa na barua zinazotambulika na wasaini bondi ya shilingi milioni 5.
Mshitakiwa Yusuph aliachiwa kwa dhamana lakini Muabhi amepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hiyo na kesi imeahirishwa hadi February 10, 2022 kwa ajili ya kutajwa