Kizimbani kwa kukutwa na chuchu za mwanamke

Mshtakiwa Salum Mkonja, anayeishi Simiyu kushoto mwenye shati jeusi akifikishwa mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi inayomkabili

Mkazi wa Maswa mkoani Simiyu nchini Tanzania, Salum Nkonja maarufu kama Emmanuel Mkonja , amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es salaam akikabiliwa na kesi ya Uhujumu uchumi yenye mashitaka 11 yakiwemo ya kukutwa na sehemu za siri za mwanamke na nyara za serikali. 

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Caroline Matemu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Ramadhani Rugemalila imedaiwa kuwa mshtakiwa alikutwa na kosa hilo Oktoba 30, mwaka 2017, katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam,.

Katika shtaka la kwanza hadi la nane kati ya Oktoba 30 na Novemba 30, 2017 huko bungo, Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki nyara za serikali zenye thamani ya Jumla ya shilimgi  20,536,555.

Amezitaja nyara hizo kuwa ni uume wa Mbwamwitu wenye thamani ya shilingi 2,272,600, uume wa Nyumbu wenye thamani ya shilingi 1,477,450, mikia mitano ya ngiri yenye thamani ya shilingi 5,114,250 na uume wa fisi mitatu, yenye thamani ya shilingi 3,750,450.

Pia alikutwa akimiliki yai moja la Mbuni lénye thamani ya sh 2,827,600, ngozi moja iliyokaushwa ndege aina ya Ngekewa mwenye thamani ya shilingi 227,300 na kichwa kimoja cha nyoka aina ya Kobra chenye thamani ya shilingi 193,205.

Pia mshtakiwa Mkonje anadaiwa kukutwa akimiliki viungo vya binadamu ambavyo ni sehemu za siri za mwanamke tano, mafuvu mawili ya binadamu na chuchu tano za mwanamke.

Hata hivyo mshtakiwa amekana kukutwa na viungo hivyo na amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo yalimtaka kuwa na wadhamini wawili waliopaswa kusaini bondi ya shilingi Milioni tano.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo umeshakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Juli 5, 2022 itakapokuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali na kesi kuanza kusikilizwa.