Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Kenya, KNCHR imekanusha usemi wa Rais William Ruto kuhusu takwimu zilizokusanywa katika eneo la Githurai, Nairobi wakati wa maandamano
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa KNCHR Roseline Odede, tume hiyo inasema imefahamishwa kuhusu usemi wa Rais Ruto wakati wa mahojiano na vituo vya televisheni kenya kwamba ilitoa data gushi kuhusu mauaji ya Githurai.
Tume hiyo sasa inafafanua kwamba bado haijatoa taarifa kuhusu mauaji ya Githurai na kwamba walipotoa taarifa, walisema wazi kwamba hawakuwa na ufahamu kamili wa matukio ya maeneo ya Githurai, Rongai, Migori, Nakuru na mengine nchini wakati wa maandamano, yalioongozwa na Vijana wa kenya
Imeelezea pia kwamba data waliyonayo inaonyesha kwamba idadi ya vifo kutokana na maandamano ilikuwa ni 22 kufikia siku ya Jumatano walipotoa taarifa hiyo.
Kufikia jana Jumapili, tume hiyo inasema ilikuwa na ufahamu wa jumla ya vifo 24 vilivyonakiliwa tangu maandamano yalipoanza kufikia sasa.
Huku ikiahidi kuendelea kutetea haki za binadamu, KNCHR imetoa pole kwa waliofiwa na jamaa wao na kuwatakia waliopata majeraha uponyaji wa haraka.