Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Tanzania(DCEA) imewakamata watuhumiwa 11 akiwemo kocha wa makipa wa timu ya Simba Club, Muharami Sultan (40) anayetuhumiwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin na bangi.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya ametoa taarifa hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo mbali na Muharami Sultani anayedaiwa kukutwa na kilo 34.89 za dawa za kulevya aina ya heroin na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa ya kulevya aina ya bangi, wengine waliotajwa ni pamoja na mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zuberi seif, Said Matwiko mkazi Magole.
Wengine ni Maulid Mzungu maarufu mbonde (54) mkazi wa kisemvule na John John maarufu Chipanda (40) ambaye jukumu lake kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy.
Wengine ni Rajabu Dhahabu (32) mkazi wa Tabata, Seleman Matola Said (24) mkazi wa Temeke Wailes, Hussein Pazi (24) na Ramadhani Chalamila (27).