KODI YA MAJENGO KWA NJIA YA UNUNUZI WA UMEME KUANZA Agosti 20,2021 TANZANIA

Serikali imesema inaanza utekelezaji wa kukusanya kodi ya majengo kwa mfumo mpya wa ukusanyaji kupitia ununuzi wa umeme. Zoezi hilo linaanza rasmi kesho Agosti 20,2021 na unafanyika chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania ukihusisha mita zote za umeme.Utaratibu huu unafanyika kufuatia marekebisho ya sheria ya kodi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa sura 289 iliyopitishwa na Bunge la Bajeti 2021 ambapo viwango vya kodi ya majengo vimebadilishwa.

Utekelezaji wa kukusanya kodi ya majengo kwa mfumo mpya.

Njia hii mpya ya ukusanywaji wa kodi imefafanuliwa kuwa kila mnunuzi wa umeme atakatwa shilingi 1000 kwa mwezi kwa nyumba ya kawaida na shilingi elfu 5000 kwa mwezi kwa kila sakafu ya ghorofa.Serikali imesema kwa wale wanaotumia mita za Ankara watalipa kodi hii kwa pamoja katika Ankara ya mwezi.


Kwa wamiliki ambao majengo yao hayajapata umeme wataendelea kulipa kodi hiyo kwa kutumia mfumo uliokuwa unatuma hapo awali, ambao ni kwa njia ya asimu au kulipa kwa njia ya benki.Kodi ya Majengo ilikuwa ikikusanywa na Mamlaka ya Serikali za mitaa lakini mwaka 2016/17 jukumu la ukusanywaji wa kodi hiyo ilihamishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), na hadi sasa mamlaka hiyo inaendelea kusimamia jukumu hilo.