Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA limesema kuongezeka kwa mgogoro nchini Ukraine kunaleta tishio la haraka na linaloongezeka kwa maisha na ustawi wa watoto milioni 7.5 wa nchi hiyo.
Mbali na kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu UNFPA ilibainisha kuwa watoto wameuawa, kujeruhiwa, na wanatiwa kiwewe sana na ghasia zinazowazunguka. Mamia kwa maelfu ya watoto wametenganishwa na familia zao na kukimbilia nchi jirani kusaka hifadhi.
Kila uchwao idadi ya wakimbizi kutokea Ukraine inaendelea kuongezeka wakikimbilia katika nchi jirani za Poland, Hungary, Moldova, Romania, Slovakia, na nchi nyingine za Ulaya.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, Ukraine ina wastani wa wajawazito 265,000, kati yao wapatao 80,000 wanatarajiwa kujifungua katika kipindi cha miezi mitatu ijayo na hivyo kuna uhitaji wa haraka wa kuongeza juhusi za kuokoa maisha ili kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wote wanalindwa dhidi ya ukatili, na watoto wanazaliwa salama na kwa uangalifu wa hali ya juu.
Shirika hilo linasambaza vifaa muhimu kwa wanawake ikiwemo taulo za kike.