Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imezitaka shule zote nchini kuwasilisha orodha ya mabasi yanayotumika kubeba wanafunzi, sambamba na majina, namba za Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na leseni za madereva wake, ili wasajiliwe kwa lengo la kuongeza udhibiti.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa matukio ya kuwafanyia vitendo vya ukatili na ukiukwaji wa maadili na udhalilishaji kwa wanafunzi unaofanywa kwenye mabasi ya shule.
Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mamlaka hiyo kudhibiti ukiukwaji wa maadili katika vyombo vya usafiri na biashara.
Akizungumzia ukiukwaji wa maadili katika mabasi ya shule, Suluo alisema – zipo taarifa za watoto wa shule kunajisiwa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ndani ya mabasi hayo na kuwa viongozi wa serikali na jamii walishalizungumzia na wao kama wadhibiti wanataka sheria ifuatwe.
“Ukiukwaji mkubwa wa maadili na matukio ya kunajisiwa watoto wa shule katika mabasi ya shule zipo, Waziri Mkuu alishalisemea na waziri anayehusika na watoto pamoja na viongozi wa dini, sisi sheria zetu ziko wazi, tunataka wamiliki wa shule nchini kote wazitekeleze,” alisema Suluo.