Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania(LHRC) kimitaka vyombo vya ulinzi na usalama na mamlaka za kisheria kuhakikisha vinafuata sheria pindi vinapomkamata mtu au watu ikiwemo kuwafikisha Mahakamani ndani ya muda unaokubalika kisheria.
Kauli ya kituo hicho imekuja siku moja baada ya tukio la kutekwa na kupigwa kisha kutupwa porini Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) Aisha Machano ambaye sasa anauguza majeraha yaliyotokana na kipigo.
Mkurugenzi wa LHRC Anna Henga amesema siku za hivi karibuni kupitia taarifa mbalimbali kutoka kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kumeshuhudiwa taarifa za uwepo wa matukio ambayo amedai kuwa yanaonekana kukiuka misingi ya ‘Haki za Binadamu na Utawala Bora, ikiwemo vitisho na matukio ya watu kutekwa huku wengi wakionekana ni wanasiasa hasa siasa za upinzani akitolea mfano tukio la kutekwa kwa Aisha Machano.
“Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa yeye mwenyewe Bi Aisha alibainisha kuwa mnamo tarehe 19 Oktoba 2024 akiwa katika kituo cha daladala wilayani Kibiti alivamiwa na wanaume sita na mwanamke mmoja waliojitambulisha kuwa ni maafisa wa Jeshi la Polisi na kisha kumkamata, taarifa hiyo inadai kuwa Bi Aisha aliteswa na kufhalilishwa kijinsia na hatimaye kupoteza fahamu kisha kumtelekeza maporini” –Dkt. Henga.
Aidha, LHRC imelaani vikali vitendo vya kukamatwa na kuumizwa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia, haswa ikizingatiwa kuwa muathirika wa tukio tajwa ni mwanamke.
Kituo hicho kimeendelea kusisitiza kuwa vitendo vya kunyanyasa na kuumiza wanawake hususani wanaojihusisha na siasa katika kipindi hiki cha uchaguzi havikubaliki kwani ni kinyume na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama wake.
Pia, LHRC imetoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuwasaka, kuwatia mbaroni na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watendaji wa matukio ya aina hiyo ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.