Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akikabiliwa na jumla ya mashtaka manne, likiwemo la uhaini, ambayo kwa pamoja yameibua mjadala mzito kuhusu uhuru wa kisiasa nchini.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, wilayani Mbinga mkoani Ruvuma muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara. Usiku huo huo alisafirishwa kwa magari hadi Dar es Salaam na kufikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central), kabla ya kupelekwa mahakamani leo asubuhi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, Gaston Garubindi, Lissu alifika kituoni saa nne asubuhi na alielezwa kuwa anakabiliwa na makosa manne likiwemo la uhaini, pamoja na makosa matatu ya kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo zenye lengo la kuchochea chuki na kupotosha umma.
“Polisi wanasema wanamtuhumu kwa makosa manne: kosa la kwanza ni uhaini, la pili, tatu na nne ni kuchapisha taarifa za uongo zenye madhara kwa usalama wa taifa,” alisema Garubindi mbele ya waandishi wa habari.
Maelezo ya Mashtaka Mengine Matatu
Mbali na shtaka la uhaini, Lissu pia anakabiliwa na mashtaka yafuatayo:
- Kuchapisha taarifa za uongo kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 – Ambapo inadaiwa alidai kwamba wagombea wa CHADEMA walienguliwa kwa maelekezo ya Rais. Serikali inadai kuwa alijua taarifa hiyo ni ya uongo na ilikuwa na lengo la kupotosha umma na kuharibu taswira ya mamlaka ya juu ya nchi.
- Kutoa kauli ya kuhusisha Polisi na wizi wa kura – Lissu anadaiwa kunukuliwa kwenye YouTube akisema: “…Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi…”. Serikali inasema kauli hiyo ni ya uongo na inalenga kupotosha raia dhidi ya vyombo vya dola.
- Kudhalilisha Mahakama – Katika shitaka la nne, Lissu anadaiwa kusema: “…Majaji ni ma-CCM hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa…” ambayo pia inatajwa kuwa ni kauli ya kupotosha na kudhoofisha heshima ya mhimili wa mahakama.
Mashtaka ya Uhaini Yasomwa Kisutu
Katika hati ya mashtaka ya uhaini, upande wa mashtaka umeeleza kuwa mnamo Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, Lissu alinukuliwa akisema:
“…walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli,… kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hiyo ndiyo namna ya kupata mabadiliko… huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli… tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Serikali inadai kuwa kauli hiyo ilikusudia kuchochea umma kuzuia uchaguzi na kuhatarisha amani ya taifa, jambo linalokiuka sheria na kuhusishwa na uhaini.
Kesi yapigwa kalenda, dhamana yazuiliwa
Baada ya kusomewa mashtaka, Mahakama ya Kisutu imepiga kalenda kesi hiyo hadi Aprili 24, 2025, kwa ajili ya kutajwa. Kwa kuwa kosa la uhaini ni miongoni mwa makosa makubwa, mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana. Lissu atasalia rumande hadi kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa rasmi.
Upande wa utetezi unaongozwa na jopo la mawakili mashuhuri wakiwemo Dk. Rugemeleza Nshalla, Hekima Mwasipu, Jebra Kambole, Dickson Matata, Gaston Garubindi na Michael Lugina.
Chadema yahoji uhalali wa kesi, yaomba msaada wa kimataifa
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, CHADEMA imekosoa vikali hatua ya kumfungulia Lissu mashtaka ya uhaini, wakidai ni jaribio la kisiasa la kunyamazisha sauti ya upinzani.
“Tunalaani vikali kuhusishwa kwa mwenyekiti wetu na kesi ya uhaini kwa kauli za kisiasa. Tunaomba msaada kutoka kwa wanasheria wa ndani na nje ya nchi kushirikiana nasi kumtetea Mheshimiwa Lissu katika kesi hii ya kisiasa,” imesema sehemu ya taarifa ya chama hicho.
Polisi Wazuia Mkutano wa Hadhara Ruvuma
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limetangaza kusitisha mikutano yote ya CHADEMA, ikiwemo ule uliopangwa kufanyika leo Aprili 10, 2025 katika uwanja wa Matalawe mkutano wa kuhitimisha ziara ya siku sita ya viongozi wa chama hicho katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, amesema walipokea barua rasmi kutoka kwa polisi ikiwataka wasitishe mara moja mkutano huo uliotarajiwa kuhutubiwa na Lissu kabla ya kukamatwa kwake.