Lissu Aibua hoja Kuhusu Uchaguzi na Tuhuma za Uhaini

Tundu Lissu ameendelea kuhoji ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya uhaini inayomkabili kwa kuangazia uhusiano kati ya hotuba yake kuhusu uchaguzi mkuu na tuhuma za uhaini zinazomkabili.

Lissu Aibua hoja Kuhusu Uchaguzi na Tuhuma za Uhaini

Katika mahojiano yake ya maswali ya dodoso kwa shahidi, Lissu alitaka shahidi aeleze iwapo hotuba yake ilikuwa ikizungumzia masuala ya uchaguzi na changamoto za mfumo wa uchaguzi nchini.Shahidi alikubaliana na Lissu kwamba hotuba hiyo ilihusu uchaguzi mkuu na matatizo yanayohusiana na uchaguzi.Lissu kisha alimuuliza shahidi iwapo Katiba inaeleza kwamba mtu anayekusudia kuvuruga uchaguzi anapaswa kushtakiwa kwa kosa la uhaini.Shahidi alijibu kuwa Katiba haijaeleza hivyo.Lissu pia alimuuliza kama katika hotuba hiyo alitishia Mahakama au Bunge. Shahidi alijibu “hapana” kwa maswali yote mawili.Katika hatua nyingine, Lissu alitaka kujua ni chombo gani kinachosimamia uchaguzi nchini. Shahidi alijibu kuwa ni Tume ya Uchaguzi.Lissu kisha akauliza kama katika maneno yaliyotumika katika shtaka lake alilitaja Tume ya Uchaguzi. Shahidi akajibu kuwa hakulitaja.Lissu pia alisisitiza kuwa katika hotuba yake aliikosoa vikali mifumo ya uchaguzi, ikiwemo namna Tume ya Uchaguzi inavyoundwa na kile alichodai kuwa ni upendeleo kwa Chama Cha Mapinduzi, CCM.Shahidi alikubaliana na maelezo hayo.Kwa upande mwingine, Lissu alimuuliza shahidi kuhusu madai kwamba yeye ndiye aliyechapisha video inayodaiwa kuwa sehemu ya ushahidi wa mashtaka kwenye akaunti ya Jambo TV.Shahidi alisema ni sahihi kwamba Lissu ndiye aliyechapisha video hiyo, lakini alipoulizwa kama Lissu ni mfanyakazi wa Jambo TV, mpiga picha au mtangazaji wa kituo hicho, alisema hana uhakika.Pia alisema hana uhakika kama Lissu alikuwa na uwezo wa kuingia kwenye mtandao wa Jambo TV.Maswali hayo yameelekezwa katika kuhoji msingi wa madai kwamba Lissu ndiye aliyehusika na uchapishaji wa video inayohusishwa na tuhuma za uhaini.Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa, huku ikiwa tayari mashahidi 15 upande wa Jamhuri wakiwa tayari wamemaliza kutoa ushahidi wao na sasa Amini Mahamba ambaye ndiye mpelelezi Mkuu wa kesi hii akiwa ni shahidi wa 16 kati ya mashahidi 30 wa Jamhuri.