Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Antiphas Lissu
Mwenyekiti wa Chadema na mwanasiasa maarufu wa upinzani, Tundu Antiphas Mughwai Lissu, akiwa gerezani Ukonga, amelaani vikali mashambulizi aliyoyaita ya kigaidi dhidi ya Padre Dkt. Charles Kitima na mdau wa demokrasia, Mdude Nyagali.
“Ninalaani kwa maneno makali kabisa shambulio dhidi ya Padre Dkt. Charles Kitima na kipigo pamoja na mateso yanayoendelea dhidi ya Mdude Nyagali,” alisema Lissu katika taarifa yake. “Naiwajibisha moja kwa moja Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa matukio haya ya kikatili.”
Lissu alitoa wito huo akiwa gerezani ambapo anashikiliwa kwa makosa ya Uhaini na Uchochezi ambapo ameitaka serikali kuhakikisha kuwa Nyagali anaachiwa mara moja na kupata matibabu ya haraka kutokana na hali yake ya kiafya.

Kuhusu Padre Kitima, Lissu alimtakia nafuu ya haraka na kuwasihi maaskofu wa Tanzania kuendelea kusimama kidete katika kupigania haki, usawa, na demokrasia.
Aidha, Lissu aliwatia moyo viongozi, wanachama, na wafuasi wa CHADEMA pamoja na Watanzania kwa ujumla kuendelea na harakati za kudai demokrasia. Alisisitiza kuwa hata kifungo hakitavunja moyo wake wala msimamo wake usiotetereka.
“Nawapenda wote, na nitarudi,” alisema.
Katika hitimisho la ujumbe wake, Lissu aliongeza kuwa iwapo hatapelekwa mahakamani siku ya Jumanne kama inavyotakiwa kisheria, ataanza mgomo wa kula.