Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ametoa malalamiko yake dhidi ya kile alichokitaja kuwa ni matumizi mabaya ya Mahakama, kufuatia kucheleweshwa kwa hatua za kisheria katika kesi ya uhaini inayomkabili, akieleza kuwa ucheleweshaji huo unadhoofisha misingi ya haki, sheria na usawa mbele ya sheria.
Katika kesi hiyo iliyopo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga , Lissu amedai kwamba kuendelea kwa hatua za kuahirisha kusomwa kwa shauri hilo ni dhihirisho la namna vyombo vya sheria vinavyoweza kutumiwa kisiasa, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa demokrasia nchini.
Kesi hiyo ya uhaini dhidi ya Lissu ilifunguliwa Aprili 2025, ambapo anadaiwa kutoa kauli zinazotafsiriwa na upande wa Jamhuri kuwa ni uchochezi wa kuleta uasi dhidi ya dola.
Tangu kufunguliwa kwake, kesi hiyo haijasogezwa mbele, huku upande wa mashtaka ukieleza kuwa unakamilisha baadhi ya taratibu za kisheria kabla ya kuwasilisha rasmi hati ya mashtaka Mahakama Kuu.
Leo, kesi hiyo ilitajwa kwa mara nyingine mbele ya Hakimu Mkazi Franco Kiswaga, ambapo upande wa Jamhuri uliomba kuahirisha shauri hilo hadi Agosti 13, 2025, kwa kuwa bado unasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu juu ya maombi ya kulinda mashahidi
Hoja za Lissu na malalamiko yake
Lissu, ambaye anajitetea mwenyewe katika kesi hiyo, alieleza kuwa kucheleweshwa kwa kesi hiyo kwa kisingizio cha kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu ni njama za wazi za kumnyima haki ya kupata haki kwa wakati.
“Haya maombi yasiyoisha ya kuahirisha kesi ni matumizi mabaya ya Mahakama. Hii inatokea kwa sababu Mahakama imekubali hali hii,” alisema Lissu kwa msisitizo mkubwa.
Aliongeza kuwa hadi kufikia leo, ameshikiliwa kwa siku 112 bila shauri lake kuendelea mbele kwa hatua zingine za kisheria, jambo ambalo ni kinyume na amri ya awali ya mahakama hiyo, iliyotaka hati hiyo iwasilishwe tarehe 30 Julai.
“Ninaishi mahabusu na wafungwa waliohukumiwa kifo. Wameniweka huko ili nianze kuzoea mazingira hayo”- alisisitiza Lissu kwa uchungu.
Akiwa na rejea ya moja kwa moja ya kisheria, Lissu alinukuu kifungu cha 262(6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Rejeo la 2025), ambacho kinaitaka Jamhuri kuwasilisha hati ya mashtaka Mahakama Kuu mara tu uchunguzi unapoisha. Kwa mujibu wa Lissu, kucheleweshwa kwa hatua hizo za kisheria ni ushahidi kuwa kuna maslahi ya kisiasa yanayoingilia mwenendo wa haki.
Kwa upande wake, Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga alieleza kuwa maombi ya kulinda mashahidi ni ya kisheria na ni sehemu ya kulinda usalama wa mashahidi katika kesi hiyo, hivyo ni muhimu kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu.
“Tunasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu maombi ya kulinda mashahidi kabla ya kuendelea na hatua nyingine. Huu ni utaratibu wa kawaida unaozingatia sheria,” alisema Katuga.
Hata hivyo, Mahakama haikutoa uamuzi wowote wa moja kwa moja kuhusu ombi hilo la kuahirisha, ambapo Hakimu Mkazi Kiswaga alisema kuwa hoja zote zilizowasilishwa zinahitaji kufanyiwa utafiti wa kina wa kisheria kabla ya kutoa uamuzi wowote.
Kesi hiyo sasa imeahirishwa hadi Agosti 13, 2025, ikisubiri uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu maombi ya kulinda mashahidi. Hatima ya shauri hili inaweza kuwa na athari pana, si tu kwa Lissu binafsi, bali pia kwa imani ya wananchi katika taasisi za utoaji haki na utawala wa sheria kwa ujumla.
.