Lissu aomba kesi yake isikilizwe haraka kwa hofu ya afya

 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameiomba Mahakama ya Rufani Tanzania, kuharakisha usikilizwaji wa shauri la mapitio ya jinai lililofunguliwa dhidi yake na Jamhuri.

Shauri hilo la mapitio ya jinai namba 7203216/2026 lilifunguliwa Februari 24, 2026, likitokana na uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu. Katika uamuzi huo, Mahakama Kuu iliikatalia Jamhuri kuwasilisha ushahidi mpya wa mmoja wa mashahidi wake.

Kutokana na kutoridhishwa na uamuzi huo, Jamhuri iliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Rufani ikiomba mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu.

Katika majibu yake ya maandishi pamoja na kiapo cha kupinga maombi hayo, Lissu pia amewasilisha hati ya dharura akiomba shauri hilo lisikilizwe kwa haraka.

Ameeleza sababu tano kuu, ikiwemo kuwa yuko kizuizini tangu Aprili 2025, pamoja na hali yake ya afya inayohitaji uangalizi wa mara kwa mara kufuatia jaribio la mauaji dhidi yake mwaka 2017.

Aidha, Lissu amesema kuwa kutokana na kuwepo gerezani ameshindwa kuhudhuria matibabu yake ya mara kwa mara, hali inayoweza kuhatarisha afya yake. Ameonya kuwa kucheleweshwa kwa usikilizwaji wa shauri hilo kunaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kiafya.

“Naiomba Mahakama hii ithibitishe ombi hili kuwa la dharura na kuelekeza lisikilizwe mapema iwezekanavyo,” amesema Lissu.

Katika kesi ya msingi, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru.