
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imekataa kupokea kama kielelezo taarifa ya uchunguzi wa picha jongefu (video) iliyowasilishwa na shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi, Oktoba 23,2025 na jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Danstan Ndunguru, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili kuhusu pingamizi lililowekwa na Lissu, ambaye anajitetea mwenyewe.
Katika pingamizi hilo, Lissu alipinga uwasilishaji wa taarifa hiyo akieleza kuwa shahidi, Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Samwel Elibariki Kaaya hana mamlaka ya kisheria ya kuandaa “report” bali “certificate” pekee ya uchunguzi, kwa mujibu wa tangazo la serikali linalomtambua chini ya kifungu cha 216(1) cha Sheria ya Ushahidi.
Mahakama imekubaliana na hoja za Lissu, ikisema kuwa shahidi huyo, kama mtaalamu aliyeteuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) au Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), anapaswa kuandaa “certificate” na si “report.”
Aidha, imeeleza kuwa kukubalika kwa taarifa hiyo kungepingana na uamuzi wake wa awali wa kukataa kupokea “flash disk” na “memory card” kama vielelezo.
Baada ya uamuzi huo, kesi inaendelea kwa Lissu kuanza kumuuliza maswali ya dodoso (cross examination) shahidi huyo wa tatu wa Jamhuri.