Lissu atumia saa 7 kumuhoji shahidi wa Jamhuri katika kesi ya uhaini

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu inatarajiwa kuendelea kesho katika Mahakama Kuu, ambapo upande wa Jamhuri unatarajiwa kusawazisha hoja na maswali ya dodoso yaliyoulizwa na Lissu kwa shahidi wa pili wa upande huo, kabla ya kuwasilisha shahidi mwingine.

Leo, upande wa mshtakiwa ambaye anajitetea mwenyewe uliendelea kumhoji kwa kina shahidi wa kwanza wa Jamhuri ACP George Bagemu ambaye ni afisa wa polisi aliyewahi kuwa RCO wa Rufiji mwaka 2018.

Katika mahojiano hayo, Lissu alitumia takribani saa saba kumuhoji Shahidi huyo kuanzia majira ya saa 3:30 mpaka saa 10, muda wote aliutumia kupima uhalali wa ushahidi wa shahidi huyo, akihusisha masuala  mbalimbali kulinga na ushahidi aliouandika katika maelezo yake ikiwamo ya taratibu za kiuchunguzi, matumizi ya notebook ya polisi, video za ushahidi na tafsiri ya maneno yaliyotumika kwenye mashtaka ya uhaini.

Lissu alihoji iwapo shahidi huyo aliwasilisha notebook aliyotumia wakati akichukua maelezo ya polisi, jambo ambalo shahidi alikiri hakulifanya. Pia alimuuliza kuhusu video iliyotajwa kama ushahidi, na kama kulikuwa na uchunguzi wa kisayansi uliothibitisha uhalisia wake. Shahidi alikiri hajaisoma ripoti ya kitaalamu ya uchunguzi huo, lakini alisema video “itawasilishwa baadae.”

Katika sehemu nyingine, Lissu alimtaka shahidi atafsiri maneno “uasi” na “tutakinukisha vibaya sana,” akisema kwamba maneno hayo yamekuwa msingi wa shtaka la uhaini. Hata hivyo, shahidi alisema hakuandika tafsiri ya moja kwa moja, na kudai kuwa “kukinukisha vibaya” ni kosa la uhaini kwa mujibu wa uelewa wake wa kijeshi.

-PGO na Haki za Binadamu-

Lissu pia alinukuu Police General Orders (PGO) akimtaka shahidi akiri kwamba polisi wanapaswa kuheshimu haki za binadamu, uhuru wa maoni, na demokrasia. Shahidi alikubaliana na maelezo hayo, lakini akakataa kusema moja kwa moja kwamba Lissu na chama chake walikuwa na haki ya kukutana au kupinga serikali.

Lissu: Nataka nikurudishe kwenye PGO (Police General Orders). Ni kweli kwamba askari polisi wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuelewa kuwa wanayafanya kwa kuzingatia kanuni na misingi ya demokrasia?
Shahidi: Kweli.

Lissu: Ni kweli kwamba askari wanatakiwa kuheshimu haki za binadamu na uhuru uliowekwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wote wa utendaji wao wa kazi?
Shahidi: Sahihi.

Lissu: Na ni kweli kwamba hayo niliyoyasema yapo kwenye Order No. 1 Paragraph 3 ya PGO?
Shahidi: Kweli.

Lissu: Sasa nataka uelewe kwamba miongoni mwa haki ambazo polisi wanatakiwa kuziheshimu ni pamoja na haki ya kutoa maoni.
Shahidi: Sahihi.

Lissu: Ni kweli kwamba PGO inatamka wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na inayoheshimu uhuru wa vyama vya siasa?
Shahidi: Ni kweli.

Lissu: Ni kweli au si kweli kwamba ni haki kwa mtu yeyote kupinga Serikali iliyopo madarakani?
Shahidi: Ni kweli.

Lissu: Nataka uwaeleze Waheshimiwa Majaji, je, katika maelezo yako kuna mahali popote ulieleza kwamba huyu Tundu Lissu na chama chake, Chadema, wana haki ya kukutana na kuzungumza masuala yao ya kupinga Serikali au kuhusiana na uchaguzi?
Shahidi: Hakuna.

Lissu: Kuna mahali popote ambapo uliandika kwamba Tundu Lissu na wenzake wana haki ya kukosoa utendaji wa majaji wa nchi hii?
Shahidi: Hakuna.

Lissu: Kuna mahali popote katika maelezo yako ambapo uliandika kwamba Tundu Lissu na wenzake wana haki ya kusema majaji hawa ni wa CCM?
Shahidi: Hakuna.

Katika hoja za kisiasa, Lissu aliorodhesha nyadhifa zake mbalimbali ikiwemo kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mwanasheria Mkuu wa Chadema, na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, akisisitiza kuwa kesi hii inamgusa mtu mwenye nafasi kubwa kitaifa. Hata hivyo, shahidi alisema “umuhimu wake si wa kipekee.”

Lissu: Kwa mujibu wa PGO namba 6, kifungu cha 16 Appendix C, tulikubaliana kwamba hii ni kesi ya umuhimu mkubwa kwa umma.
Shahidi: Ni sawa.

Lissu: Ni kesi inayomuhusu mtu muhimu kisiasa kama mshtakiwa?
Shahidi: Si kweli, sioni huo umuhimu.

Lissu: Ni kweli kwamba mshtakiwa katika kesi hii ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani?
Shahidi: Si kweli.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, huyu mshtakiwa kwenye kesi hii ni Makamu Mwenyekiti na mjumbe wa Kamati ya IDU?
Shahidi: Sifahamu.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, kama unafahamu au hufahamu kwamba alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA?
Shahidi: Sahihi.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, mshtakiwa katika kesi hii aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA kati ya mwaka 2011 hadi 2017, baada ya mimi kupigwa risasi.
Shahidi: Najua ulikuwa Mwanasheria Mkuu, hilo la kupigwa risasi sijui.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, kama unafahamu kwamba mshtakiwa huyu aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Sheria wa CHADEMA kuanzia mwaka 2004 hadi 2010.
Shahidi: Nafahamu.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, kama unafahamu kwamba mshtakiwa huyu aliwahi kuwa Mbunge.
Shahidi: Nafahamu.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, kama unafahamu kwamba mshtakiwa huyu aliyepo mbele aliwahi kuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuanzia mwaka 2010 hadi Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa akiwa bungeni.
Shahidi: Hilo nalijua.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, kama unafahamu kwamba mshtakiwa huyu aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu Kivuli Bungeni kati ya mwaka 2010 hadi 2017, aliposhambuliwa kwa risasi akiwa bungeni.
Shahidi: Hilo la Mwanasheria nalifahamu, hilo la risasi liondoe.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, kama unafahamu kwamba mshtakiwa huyu aliwahi kuwa Waziri Kivuli wa Sheria kati ya mwaka 2010 hadi 2017, hadi aliposhambuliwa kwa risasi bungeni.
Shahidi: Ninatambua kama alikuwa Waziri Kivuli.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, kama unafahamu kwamba mshtakiwa huyu aliwahi kuwa Waziri Kivuli wa Masuala ya Muungano kati ya mwaka 2010 hadi 2017, aliposhambuliwa kwa risasi akiwa bungeni.
Shahidi: Sifahamu.

Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, kama umewahi kusikia kwamba mshtakiwa huyu aliyepo mbele aliwahi kushambuliwa kwa risasi bungeni na watu wasiojulikana.
Shahidi: Najua ulishambuliwa, kuhusu hao wasiojulikana na idadi ya risasi sijui.

Lissu anashtakiwa kwa kesi ya Uhaini chini ya kifungu cha sheria ya makosa ya jinai cha 39(2d) ambapo kwa mujibu wa sheria mshtakiwa akikutwa na hatia adhabu yake ni kunyongwa.

Anadaiwa kutoa mananeo yanayoashiria Uhaini kupitia mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Aprili 4, 2025 katika wilaya ya Kinondoni.

Kesi hiyo leo imeahirishwa mpaka kesho Oktoba 9,2025 ambapo Mahakama inatarajia kuendelea na ushahidi kwa Jamhuri kusawazisha majibu ya maswali ya dodoso yaliyoulizwa na Lissu leo, kabla ya kuendelea na shahidi mwingine wa pili katika mfululizo wa ushahidi.

Mawakili wa Serikali wanatarajiwa kuwasilisha hoja za kufafanua maeneo ambayo shahidi wa leo alihojiwa kwa undani na utetezi, hususan kuhusu video ya ushahidi, tafsiri ya maneno ya “uasi,” na uhalali wa hatua za uchunguzi zilizochukuliwa.

Kesi hiyo inaendelea chini ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu, wakiongozwa na Jaji Dastan Nduguru.