Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, leo ametoa hoja mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania akipinga lugha inayotumiwa na upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Lissu alieleza kutoridhishwa kwake na namna Wakili wa Serikali alivyomtaja kama “mwenzetu”, akisisitiza kuwa hana uhusiano wowote na upande huo wa mashtaka, na kwamba alikuwa analitumia mara kwa mara
“Jambo la kwanza ambalo huenda linaonekana dogo kwa wengine – lakini kwangu si jambo dogo, ni pale Wakili wa Serikali anaposema ‘mwenzetu, mwenzetu’. Mimi si mwenzao. Mimi ni mshtakiwa wa uhaini, ningependa aniite hivyo,” alisema Lissu.
Kauli hiyo imetolewa wakati kesi ya uhaini dhidi ya Lissu ikiendelea kusikilizwa. Mnamo Septemba 16, 2025, Lissu alihitimisha hoja zake za awali za kupinga uhalali wa mashtaka, akisisitiza kuwa ni ya kisiasa na inalenga kudhibiti yeye pamoja na harakati za upinzani nchini.
Mashtaka hayo yalifunguliwa kufuatia kauli mbalimbali alizotoa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mnamo Aprili 3, 2025, ambapo alilalamikia ukosefu wa haki na uhuru nyakati za uchaguzi.
Kesi hiyo inaendelea kuvuta hisia ndani na nje ya nchi, kutokana na nafasi ya Lissu kama mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa upinzani barani Afrika. Wakati Mahakama ikiendelea kusikiliza hoja za pande zote, wafuasi wa CHADEMA na wadau wa haki za binadamu wanafuatilia kwa karibu mwenendo wake.