Mwanasiasa wa upinzani na wakili wa kujitegemea, Tundu Lissu, ameibua hoja nzito mbele ya Mahakama Kuu akipinga uhalali wa hati ya mashtaka inayomkabili katika kesi ya uhaini. Lissu anasisitiza kuwa nyaraka za mashtaka hazioneshi kosa la jinai, na hivyo haziwezi kisheria kufungua mashauri dhidi yake.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Lissu anatuhumiwa kwamba mnamo Aprili 3 alikusudia “kuchochea wananchi kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.” Hata hivyo, mwanasiasa huyo mashuhuri anasema kosa hilo haliingii kwenye wigo wa makosa ya uhaini kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
“Waheshimiwa majaji, kabla sijajibu moja kwa moja tuhuma hizo, naomba twende kwenye kifungu cha 295(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai na vilevile kifungu cha 294(1). Mtaona wazi kwamba siwezi kujibu ndiyo au hapana mpaka iamuliwe kwanza kama hii hati ya mashtaka ni halali, kwa sababu haionyeshi kosa la uhaini.”
Kwa mujibu wa Lissu, tofauti kubwa ipo kati ya hati ya mashtaka aliyoisomewa Aprili 10 na taarifa ya mashtaka aliyopewa Agosti 18. Tofauti hizo, anasema, zinaonesha nyaraka zimefanyiwa marekebisho kinyume na masharti ya kisheria.
“Hoja yangu inabaki palepale: hakuna kosa la jinai linaloonekana katika nyaraka hizo. Kwa maana hiyo hakuna kosa la uhaini. Na kwa maneno mengine, hii taarifa ni kinyume cha kifungu cha 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai,” alisema.
-Historia ya Kesi za Uhaini Tanzania-
Lissu hakusita kukumbusha historia ya kesi za aina hiyo nchini. Alisema kesi inayomkabili si ya kwanza bali ni ya tatu kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Tanzania.
“Waheshimiwa, hii si kesi ya kwanza ya uhaini katika nchi yetu. Kesi ya kwanza ilikuwa ya Grey Likungu Makaka na wenzake, maarufu kama kesi ya kina Bibi Titi Mohamed, katika enzi za East African Court. Kesi ya pili ilikuwa mwaka 1983, kesi ya Khatibu Ghandi na wenzake dhidi ya Jamhuri. Sasa hii ya kwangu ndio kesi ya tatu.”
Kwa kurejea kesi ya Khatibu Ghandi, Lissu alisisitiza kuwa Mahakama ilibainisha wazi kwamba maneno pekee hayawezi kuunda kosa la uhaini bila vitendo vinavyoashiria mpango wa kisiasa wa kuipindua serikali au kuvunja sheria.
“Mahakama ilisema wazi kwenye kesi hiyo kwamba maneno matupu hayatendi uhaini isipokuwa vitendo. Maneno ya mtu mmoja hayaundi kosa la uhaini. Mimi nimeshtakiwa peke yangu, na maneno yangu hayawezi kuwa uhaini,” aliongeza.
-Tuhuma za “Uhasi” na “Tutakinukisha”-
Katika hati ya mashtaka, Lissu anadaiwa kutumia maneno “tutahamasisha uhasi” na “tutakinukisha sawa sawa” katika mkutano wake na waandishi wa habari. Hata hivyo, amepinga tafsiri ya maneno hayo na kuomba Mahakama izingatie maana rasmi.
“Waheshimiwa majaji, nimeletea Kamusi Kuu ya Kiswahili ya Baraza la Kiswahili Tanzania. Kwa mujibu wa kamusi hiyo, neno ‘hamasisha’ maana yake ni kumpa mtu msukumo wa kufanya jambo. Lakini linapokuja suala la ‘uhasi,’ maana yake ni kitendo cha uvunjaji wa sheria kinachofanywa na kikundi cha watu kwa lengo la kubadilisha mfumo wa kisiasa wa nchi. Maana ya pili ni kupinga wenye mamlaka au kupinga sheria na taratibu zilizopo katika taasisi au chama. Sasa, je, maneno yangu yanaashiria hayo?”
Kuhusu msemo wa pili, Lissu alionekana kukejeli tafsiri ya upande wa mashtaka:
“Neno ‘tutakinukisha sawa sawa’ kwa mujibu wa Kiswahili sanifu maana yake ni ‘kunuka’ au ‘nukia.’ Waheshimiwa, je, hiyo inaweza kuwa ushahidi wa kosa la uhaini?”
Katika hoja zake, Lissu alisisitiza kuwa kifungu cha 139 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ndicho kinachoainisha makosa ya uhaini. Kifungu hicho, amesema, hakitaji popote kwamba kuzuia uchaguzi ni kosa la aina hiyo.
“Kifungu ninachoshtakiwa nacho ni cha 139 ambacho kimeanisha makosa ya uhaini. Lakini kuzuia uchaguzi mkuu sio moja ya makosa hayo. Kwa hiyo kupanga njama za kuzuia uchaguzi au chochote cha namna hiyo sio kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za nchi hii.”
Kwa mujibu wake, upande wa mashtaka umejikita zaidi kwenye tafsiri ya kisiasa badala ya tafsiri ya kisheria.
Kesi imeahirishwa hadi kesho Septemba 16,2025 saa tatu asubuhi kwa ajili ya Lissu kuendelea kutoa hoja za pingamizi lake ambalo limeanza leo.