Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu amesema anakusudia kuishtaki kampuni ya Tigo na Serikali ya Tanzania katika mahakama ya Uingereza kufuatia kampuni hiyo kushirikiana na Serikali katika kutoa taarifa zake na kumfatilia hadi kusababisha kushambuliwa kwake.
Lissu ametoa kauli hiyo leo Septemba 25,2024 wakati akizungumza na wanahabari kufuatia taarifa iliyotoelewa na Gazeti la Guardian la London lililochapisha habari kwamba kampuni ya mawasiliano ya Tigo imehusika kutoa taarifa za Lissu bila idhini yake hadi kusababisha kushambuliwa kwake.
Amesema tayari ameshatoa idhini ya kuendelea na kesi hiyo nchini Uingereza kwa Wakili wake Robert Amsterdam, na kwamba wameamua kwenda kufungua kesi hiyo huko ili haki ipatikane huku akionesha kwamba mahakama za ndani zimekosa nguvu ya kusikiliza kesi hiyo.
“Tayari nimewasiliana na Mwanasheria wangu Amsterdam afungue kesi ya madai kwa kampuni ya Millicom (Tigo) na serikali ya Tanzania. Tumeamua tufungue kesi kwenye mahakama ya kimataifa kwa sababu Rostam Aziz alisema Jaji anaweza kupigiwa simu na akapindisha haki. Kwahiyo tutafungua kesi kwenye mahakama ya kimataifa mahali ambapo Serikali haiwezi kupiga simu kwa Jaji. Mahakama ambazo zina mamlaka ya kuzuia ndege zetu huko zinapoporuka, hadi nilipwe fidia. Bado tunajadili kiasi cha madai kutokana na madhara yaliyonipata, lakini tutadai mapesa mengi sana.” amesema Lissu kwenye taarifa yake hii leo
Inadaiwa kwamba Tigo ilitoa taarifa za simu na eneo la Lissu kwa mamlaka za Tanzania kwa muda wote wa saa katika wiki zilizotangulia kabla ya shambulio hilo lililotokea tarehe 7 Septemba 2017.
Mpango huo, ambao Tigo haudai, ulifunuliwa na Michael Clifford, aliyekuwa mchunguzi wa ndani wa kampuni hiyo, katika mahakama ya London mwezi huu. Clifford, ambaye pia ni afisa wa zamani wa Polisi wa Metropolitan, anadai kwamba alifukuzwa kazi kwa sababu ya kuibua wasiwasi kuhusu suala hilo.
Mawakili wa Clifford wamesema, “Madai ya Bw. Clifford ni kwamba alitendewa kwa njia isiyo sawa, na kufukuzwa kazi kwa sababu alifanya taarifa za siri kuhusu mambo ya umuhimu wa juu na maslahi ya umma.”
Lissu amekwenda mbali zaidi akisema kwamba mpango wa kushambuliwa kwake ulianza muda mrefu kufuatana matukio yaliyotokea kabla ya kupigwa risasi, likiwemo tukio la yeye kukamatwa na polisi hadi kuambiwa akapimwe mkojo na kwamba hadi tukio linatokea eneo la bunge ambako alipaki gari lake hapakua na walinzi sikui hiyo kama ilivyokuwa kawaida.
“Kazi ya kunifuatilia na kutrack mienendo yangu yote, ilipewa kampuni ya Tigo, ambayo ndio ilifanikisha kazi ya kutoa taarifa zangu za wapi nilipo na nafanya nini.
Na Hiyo kazi ya kunifuatilia na kujua mienendo yangu, kwa mujibu wa taarifa niliyopata kutoka London, ilianza tarehe 22 Agosti 2017, sasa nataka tutafakakari kidogo hiyo tarehe 22, mnakumbuka hadithi ya ndege ya Bombardier ya Magufuli ambayo ilikamatwa Canada? Ile taarifa ya kukamatwa kwa ndege Ile ya Air Tanzania ambayo inaitwa bombardier ya magufuli, hiyo taarifa ya kukamatwa kwa ndege niliitoa kwa waandishi wa habari tarehe 18 Agost 2017, siku mbili baadaye nikakamatwa.
Mnakumbuka habari ya kupimwa mkojo? Nikakamatwa nikalala ndani kesho yake wakanichukua tarehe 21 na kunipeleka kwa mkemia mkuu wa serikali kwenda kunipima mkojo, nilipowakatalia wakaniachilia huru, katika Kesi za magufuli nilikamatwa mara 8. Baada ya kukataa kupimwa mkojo tarehe 22 ndipo wakaanza kunifuatilia kwa kutumia njia za kielekroniki”
Lissu alishambuliwa akiwa ndani ya gari lake lililokuwa kwenye maegesho ya magari yaliyopo kwenye viwanja vya bunge. Gari lake lilipigwa risasi na alijeruhiwa vibaya. Hakuna mtu aliyepandishwa kizimbani kuhusiana na jaribio hilo la mauaji.
Serikali ya wakati huo iliyokuwa chini ya Hayati John Magufuli ilisema haiwezi kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa muhusika ambaye ni Lissu hakuwepo nchini.
“Mnafahamu kwamba serikali wakati ule kwa sababu sikuwepo nchini, serikali ya Magufuli walidai kwanza watanichunguza nitakaporudi Tanzania na nitakaporud wataanza kunichunguza lakini hawajanichunguza mpaka muda huu” amezungumza Lissu
Kampuni hiyo ya Tigo inatoa huduma za mawasiliano katika masoko yanayoibuka barani Amerika ya Kusini na pia ilikuwa ikifanya kazi katika sehemu za Afrika wakati Clifford alikuwa akifanya kazi. Inasema kwamba wakati Clifford alifukuzwa kazi, ilikuwa katika mchakato wa kupunguza shughuli zake nyingi Afrika, na hivyo nafasi yake ilikuwa isiyo na kazi.
Tigo ilisema kwamba Clifford alitakiwa kuchunguza suala la Lissu na alitoa ripoti yake kama alivyotakiwa. Baada ya kupokea ripoti hiyo, walichukua ushauri wa kisheria wa ndani, na wafanyakazi wengine walichukuliwa hatua za kinidhamu.
Kesi hii imechukua miaka minne kufika mahakamani, kutokana na juhudi za Tigo kuyafanya madai ya Clifford yasikilizwe chini ya vikwazo vya ripoti. Wakati mmoja, kampuni hiyo ilidai kwamba isipokuwa ipatiwe agizo la siri, ingeshindwa kujitetea. Ombi hilo la siri lilikataliwa mapema mwaka huu.
Msemaji wa Tigo alisema hawezi kutoa maoni kwa sababu mgogoro wa kisheria na Clifford unaendelea. Alisema kwamba tangazo la wiki iliyopita la kuondoka kwa mwenyekiti mtendaji wa Tigo, Mauricio Ramos, halihusiani na kesi hiyo.
Wanachama wa vyama vya upinzani nchini Tanzania, wamekuwa katika tishio la kisiasa licha ya kubadilika kwa uongozi mwaka 2021. Jumatatu Septemba 23,2024 , polisi walimkamata Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema na Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema na wengine zaidi ya kumi kabla ya maandamano yaliyopangwa dhidi ya mauaji na kupotea kwa wanasiasa wa upinzani.