Lissu kumtumia Rais Samia kama shahidi katika kesi yake ya Uhaini

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ametaja orodha ya mashahidi wake 15 katika kesi ya uhaini inayomkabili, akiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Miongoni mwa waliotajwa pia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Camilius Wambura, Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai, na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. Lissu pia amewataja viongozi wa kikanda wakiwemo Martha Karua, mwanasiasa na mwanaharakati kutoka Kenya, Boniface Mwangi, Mwanaharakati kutoka Kenya, Agatha Atuhaire, Mwanaharakati kutoka nchini Uganda na Dk. William Mutunga, Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya.

Hatua hiyo imezua mjadala mpana, ikizingatiwa uzito wa majina yaliyoorodheshwa, huku upande wa mashtaka ukipanga kuleta mashahidi 30, baadhi yao wakiwa wa siri.

Awali, Mahakama Kuu ilitupilia mbali mapingamizi ya Lissu kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka na maelezo ya mashahidi, ikisema hoja hizo hazina mashiko kisheria. Jaji Danstan Ndunguru alibainisha kuwa hati hiyo imekidhi vigezo vya kisheria chini ya kifungu cha 135 na 138 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Mahakama pia ilikataa ombi la Lissu la kutaka shauri hilo lirushwe mubashara, ikieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa mashahidi na kuathiri mwenendo wa ushahidi. Hata hivyo, kusikilizwa kwa wazi kutaendelea kuruhusu wananchi na waandishi wa habari kufuatilia mwenendo wa kesi.

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, mkoani Ruvuma mara baada ya mkutano wa hadhara, wakati akiendeleza msimamo wa chama chake wa “No Reforms, No Election.”

Msimamo huo, uliopitishwa na Kamati Kuu ya Chadema mwezi Desemba 2024, unasema chama hicho hakitashiriki uchaguzi mkuu iwapo hakutakuwa na marekebisho ya katiba, sheria za uchaguzi na kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.

Kesi hiyo sasa inatarajiwa kuendelea Oktoba 6, 2025 kwa hatua ya ushahidi.