Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, inaendelea kupata mvuto katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kuingia siku ya tatu mfululizo, huku mvutano wa kisheria baina ya pande mbili ukizidi kushika kasi.
Shauri hilo lilitajwa leo kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa hoja za pingamizi zilizowasilishwa na Lissu, ambapo upande wa Jamhuri ulikuwa unakamilisha uwasilishaji wake kabla ya Lissu, anayejitetea mwenyewe, kujibu hoja hizo.
Itakumbukwa kuwa jana, Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga, akiongoza jopo la mawakili wa Serikali, alihitimisha sehemu kubwa ya hoja za upande wa Jamhuri kwa kueleza kuwa pingamizi lililowasilishwa na Lissu limeletwa nje ya wakati na hivyo halina mashiko ya kisheria. Katuga aliiomba Mahakama itupilie mbali pingamizi hilo ili kesi iendelee kusikilizwa kwa mujibu wa taratibu.
Kwa upande wake, Lissu anapinga Mahakama Kuu kuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa hoja kwamba utaratibu wa kisheria katika hatua ya committal uliofanyika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haukuzingatia sheria.
Aidha, ameeleza kuwepo kwa utofauti wa nyaraka na kumbukumbu za kimahakama kati ya Kisutu na Mahakama Kuu, jambo alilodai linaathiri uhalali wa mwenendo mzima wa kesi.
Katika pingamizi lake, Lissu aliwasilisha hoja tano kuu, ikiwemo madai kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kisheria kusikiliza shauri hilo kutokana na makosa ya kitaratibu yaliyojitokeza mapema.
Ameendelea kusisitiza kuwa mapungufu hayo ya kisheria yanapaswa kuzingatiwa na kwamba hoja za upande wa Jamhuri hazijajibu msingi wa malalamiko yake.
Leo mchana, wakati akijibu hoja za Serikali, Lissu alieleza kuwa upungufu wa kisheria uliopo katika mwenendo wa kesi yake hauwezi kufumbiwa macho na Mahakama, kwani ni suala linalohusu haki ya mshtakiwa na uhalali wa mchakato mzima wa haki jinai.
Shauri hilo limeahirishwa na Mahakama hadi kesho, ambapo pande zote zinatarajiwa kuhitimisha hoja za pingamizi, kabla ya Mahakama kupanga tarehe ya kutoa uamuzi mdogo (ruling) juu ya hoja hizo.