Lissu ni ama afikishwe Mahakamani kesho ama aanze mgomo wa kula akiwa gerezani

Kesho Mei 6, Mwanasheria maarufu na mwanasiasa mkongwe Tundu Antiphas Lissu anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani kwa kesi ya uhaini na uchochezi, kesi ambayo imeibua hisia kali kutoka kwa wananchi, wanasiasa, wanaharakati wa haki za binadamu na jumuiya ya kimataifa

Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa alikamatwa tarehe 9 Aprili 2025 majira ya saa za jioni akiwa Ruvuma muda mchache mara baada ya kumaliza mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Mbinga.Usiku huo huo alisafirishwa hadi Dar es Salaam chini ya ulinzi mkali wa maofisa wa polisi na kufikishwa katika kituo cha kati cha Polisi.

Aprili 10, 2025, Lissu alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako alisomewa mashitaka mawili ya uhaini na uchochezi kinyume na sheria za nchi.

Kesi hiyo imebeba uzito mkubwa, si tu kwa sababu ya asili ya mashtaka, bali pia kwa hadhi ya Lissu kama mwanasiasa aliyejaribu kugombea urais na pia kuwa mhanga wa jaribio la kuuawa mwaka 2017aliposhambuliwa kwa risasi akiwa maeneo ya bunge la Tanzania. Tangu kufikishwa kwake mahakamani, kumekuwa na harakati nyingi za ndani na nje ya mahakama, wafuasi wake na wanaharakati wa haki za binadamu wakikusanyika kila mara kushuhudia mwenendo wa kesi.

Katika moja ya vikao vya awali, mawakili wa upande wa Jamhuri  waliwasilisha ombi la kesi hiyo kusikilizwa kwa njia ya mtandao (virtual court hearing), wakitaja sababu za kiusalama. Ombi hilo lilizua mjadala mkali ndani ya ukumbi wa mahakama, huku upande wa utetezi ukipinga kwa misingi kuwa hadhi ya kesi hiyo inahitaji uwepo wa moja kwa moja wa mshtakiwa mahakamani.

Hata hivyo mshtakiwa mwenyewe aligoma kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao akishinikiza kufikishwa Mahakamani

Kauli ya Mawakili na Hofu ya Kunyimwa Haki

Akizungumza na wanahabari nje ya mahakama, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alieleza hofu yao kuhusu mwenendo wa kesi huku akiona dalili za ukandamizwaji wa haki ya mteja wao kwani kama mawakili wa utetezi walizuiwa pia kuonana na mteja wao ambaye sasa anashikiliwa katika gereza la Ukonga Dar es salaam.

Kibatala alieleza kuwa pamoja na kwamba Lissu anashitakiwa kwa kosa la uhaini ambalo halina dhamana lakini ni haki yake kisheria kupewa faragha kuonana na mawakili wake tofauti na alivyodai Kibatala kwamba fursa hiyo ni ndogo kwao.  

“Misingi ya kawaida ya kuhudumia wafungwa iliyopitishwa na Baraza la Umoja wa Taifa inasema wafungwa wote watapewa nafasi ya kuwasiliana na mawakili au wasaidizi wao wa kisheria bila kuchelewa, magereza wana haki ya kushuhudia kinachotendeka lakini sio kusikiliza tunachoongea na mteja wetu” amesema Kibatala.

Lissu atishia mgomo wa kula

Katika kile kinachoashiria ongezeko la taharuki, taarifa zilizotolewa na timu ya mawakili wa Lissu zimedokeza kuwa mteja wao yuko tayari kuanza mgomo wa kula endapo hatapelekwa mahakamani kesho kama ilivyopangwa. “Mteja wetu amechoka kucheleweshewa haki. Ikiwa serikali itazidi kuvuta muda, atachukua hatua za amani kulalamikia hali hiyo, ikiwemo kutokula hadi haki itendeke,” alisema Wakili Kibatala

Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa mahakamani Kisutu, ambako kesho Lissu anatarajiwa kufikishwa tena kusikiliza maamuzi ya mapingamizi yaliwekwa na upande wa utetezi kuhusu kuendesha kesi hiyo kwa njia ya mtandao, lakini pia kesho ndio siku ya kutajwa kwa Kesi Uhaini mbali na ile ya uchochezi. Ikiwa ni moja ya kesi zinazovuta hisia na umakini wa kitaifa na kimataifa, hatima ya Lissu itaendelea kuwa gumzo la kitaifa kwa siku zijazo.