Kesi ya Uhaini inayomkabili mwanasiasa mashughuli nchini Tanzania, Tundu Antiphas Lissu leo imeendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, ikiwa katika hatua ya kusikiliza mapingamizi yanayohusu uhalali wa mchakato wa kushtakiwa kwake, hususani juu ya mamlaka ya Mahakama ya Kuu kuendesha shauri hilo.
Jana Septemba 8, 2025 Lissu alitakiwa kusomewa hoja za awali kuhusu tuhuma anazotuhumiwa nazo kwa mara ya kwanza, lakini mchakato huo ulishindwa kuendelea baada ya yeye mwenyewe kuibua hoja mbili za mapingamizi.
Mosi Lissu anapinga mchakato mzima wa uendeshaji wa shauri lake katika Mahakama ya Kisutu na pili anapinga Mamlaka ya Mahakama Kuu kusikiliza kesi hiyo.
Katika uwasilishaji wa hoja zake hii leo, Lissu alitoa hoja nzito akieleza kuwepo kwa tofauti kubwa kati ya rekodi mbili za kesi zinazotoka kwenye Mahakama tofauti, moja kutoka Mahakama ya Kisutu ambayo nakala yake alipelekewa gereani Ukonga na nyingine kutoka Mahakama Kuu ambayo aliipata jana akiwa mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa Lissu, rekodi ya Ukonga ina kurasa 16 pekee, huku ile nyingine ya Mahakama Kuu ina kurasa 111, jambo linaloibua maswali kuhusu uhalali na usahihi wa nyaraka hizo. Pia, alihoji kwa nini rekodi ya Ukonga haina “scanning page” wakati ile ya Mahakama inayo .
Tofauti zaidi zilizotajwa ni pamoja na:
- Tarehe za kumbukumbu yaani kumbukumbu ya Ukonga inaanza na kuishia tarehe 18 Agosti 2025 pekee, wakati ile ya Mahakama inaanza Aprili 10 hadi Agosti 18, 2025.
- Uendelezwaji wa shauri – Rekodi ya Ukonga inaonyesha kwamba “Committal Proceedings” zilianza moja kwa moja bila kuwepo ubishani, wakati kwenye rekodi ya Mahakama ukurasa wa 86 unaonesha kulikuwa na mabishano makali ya kisheria ambayo hayakuonyeshwa kwenye ile ya Ukonga.
- “Orodha ya mashahidi”– Katika rekodi ya Ukonga ukurasa wa 15, orodha ya mashahidi wa utetezi haikuandikwa, wakati walikuwepo. Vilevile, katika ukurasa wa 100 wa rekodi ya Mahakama hii, bado mashahidi wa utetezi hawakuorodheshwa.
Lissu alieleza kuwa tofauti hizi ni za msingi na zinaleta mashaka kuhusu uhalali wa mchakato mzima wa “Committal Proceedings”. Alihoji ni rekodi ipi Mahakama inapaswa kuiamini, na kwanini nyaraka kutoka chanzo kimoja ziwe tofauti kiasi hiki.
“Kwenye ukurasa wa kwanza wa rekodi ya Ukonga, inaonekana kwamba committal proceedings zilianza moja kwa moja bila chochote kabla yake. Lakini kwenye rekodi ya Mahakama hii, ukurasa wa 86, kulikuwa na ubishani mkubwa sana ambao hauonekani kabisa kwenye rekodi ya Ukonga.
Kisha, kwenye ukurasa wa 15 wa rekodi ya Ukonga, kuna orodha ya mashahidi na maneno yameandikwa “nitaita mashahidi.” Hata hivyo, mashahidi wa utetezi hawakuandikwa. Siyo kwamba hawakuwepo walikuwepo, na mimi niliwataja” alisema Lissu na kuongeza
“Vile vile, kwenye ukurasa wa 100 wa rekodi ya Mahakama hii, mashahidi wa utetezi pia hawakuandikwa.Hizo ndizo tofauti zilizopo kati ya nyaraka hizi mbili, ambazo zote zinatoka Mahakamani. Swali sasa ni: tuchukue ipi, na kwa nini zina tofauti?” alisisitiza
-Msingi wa Mapingamizi: Sheria na uhalali wa ahirisho-
Lissu pia aliibua hoja kuhusu ahirisho ya mara kwa mara ya shauri hilo. Kwa mujibu wake, kulikuwa na ahirisho 13 nyingi zikiwa hazina sababu za msingi, kinyume na kifungu cha 162 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Alitoa mfano wa ahirisho la kwanza ambalo halikukidhi vigezo vya kifungu cha 265(1), pamoja na ahirisho la tarehe 24 Aprili 2025 ambapo kulikua na mvutano mkubwa wa kisheria lakini haikuandikwa kwenye baadhi ya rekodi.
Aliendelea kueleza kuwa, hata ahirisho la tarehe 6 Mei 2025 halikuwasilisha sababu zenye mashiko, jambo lililowafanya waendelee kuomba ahirisho bila msingi thabiti, huku akidai kwamba aliwekwa katika mazingira magumu gerezani, akikabiliwa na hatari ya kuchanganywa na watu waliokwishahukumiwa kunyongwa.
Katika hoja zake, Lissu aliiomba Mahakama Kuu itamke rasmi kwamba hakukuwa na *Committal Proceedings* halali Mahakama ya Kisutu, na hivyo kuomba shauri hilo lifutwe na aruhusiwe kurejea nyumbani baada ya siku 154 akiwa gerezani.
Pia alikosoa hatua ya Hakimu wa Kisutu, Franco Kiswaga, kubadilisha maamuzi ya Mahakama Kuu yaliyotolewa tarehe 4 Agosti 2025 kuhusu ulinzi wa mashahidi, akidai kuwa hatua hiyo ni sawa na “kuendesha mashauri gizani”.
-Jamhuri yapinga mapingamizi-
Akijibu hoja hizo, Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga alisema kuwa Mahakama ya Kisutu ilikuwa na mamlaka halali ya kuendesha *Committal Proceedings*, kwa mujibu wa Sheria.
Katuga alisisitiza kuwa kosa la uhaini ambalo Lissu anatuhumiwa kulitenda lilifanyika jijini Dar es Salaam, hivyo Mahakama ya Kisutu ilikuwa na mamlaka ya kisheria.
“Hoja kwamba mtuhumiwa alitakiwa kushtakiwa Mbinga ni hoja dhaifu na ya bahati mbaya,” alisema Katuga.
Pia alikana madai kwamba nyaraka muhimu hazikutolewa kwa Lissu, akieleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 266, mshtakiwa ana haki ya kupewa nyaraka wakati wa *trial*, ambayo bado haijaanza.
Kuhusu ahirisho, alikiri kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 184 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Mahakama haiwezi kupokea shauri la jinai bila *Committal Proceedings*, lakini alisisitiza kuwa mchakato huo ulifanyika kwa kufuata taratibu.
Baada ya kuskiliza hoja za pande zote mbili jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru, kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho Septemba 10, saa tatu asubuhi.