Lissu:Mifumo ya viwango vya kodi inapaswa kuwa wazi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, Tundu Lissu amesema mifumo na viwango vya kodi inapaswa kuwa wazi ili anayelipa ajue analipa kiasi gani na anayekusanya ajue anakusanya kiasi gani.

Akiwa katika soko maarufu la Kariakoo jijini Dar es salaam Lissu amedai kuwa maamuzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na Sheria kandamizi za kodi zimekuwa mwiba kwa wafanyabiashara hao na kwamba utatuzi wake ni mabadiliko ya mifumo pekee.

 “Haya masuala yanahitaji mabadiliko ya mifumo wa ulipaji kodi na sheria zetu za kodi, vilevile yanahitaji mabadiliko ya wakusanyaji wa kodi,”

Aidha Lissu ameongeza kuwa pamoja na hayo imefika wakati wa kuondolewa kwa watendaji wasiofaa na nafasi hiyo ijazwe na watu watakaokuwa na haki.

 “Tunapaswa kubadilisha watendaji wetu wasiofaa waondolewe, watakaofaa waajiriwe, kiujumla tunahitaji watu watakaokuwa na haki,”amesema Lissu.

Ziara ya Lissu hii leo katika soko hilo ni ya kwanza tangu arejee rasmi nchini Tanzania kwa ajili ya kuendeleza harakati za kisiasa na madai ya katiba mpya.