Edward Ngoyai Lowassa, jemedali katika ulingo wa siasa nchini Tanzania kwa sasa hatunae, amerudi kwa muumba aliyemleta duniani na kama ilivyoada kwa kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke basi kifo ni lazima lakini kinachotafakarisha katika kifo ni je utakufa kifo cha aina gani, lakini pia ukifa utaacha alama gani kama kumbukumbu.
Lowassa ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri Tanzania kwa zaidi ya miongo mitatu, ni Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania aliyehudumu katika nafasi hiyo kati ya Desemba 30, 2005 na Februari 7, 2008 wakati wa uongozi wa awamu ya nne wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 Wilayani Monduli mkoni Arusha akiwa mtoto wa nne wa mfugaji Ngoyai Lowassa ambaye alifanya kazi kwa muda wa ziada akiwa tarishi katika serikali ya kikoloni.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Monduli ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa Moringe kati ya mwaka 1961 na 1967.
Baada ya elimu ya msingi alijiunga na masomo ya sekondari katika shule ya sekondari Arusha kuanzia mwaka 1968 alikohitimu kidato cha nne mwaka 1971.
Hakuishia hapo kielimu, kwani alijiunga na shule ya sekondari Milambo mkoani Tabora kwa ajili ya masomo ya kidato cha 5 na 6 kati ya mwaka 1972 na 1973 alipohitimu.
Mwaka 1977, Lowassa alifuzu na kutunukiwa shahada ya awali ya Sanaa za Maonesho kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Akiwa UDSM, ndipo alikutana na Jakaya Kikwete akisoma Uchumi, na miaka zaidi ya 20 baadaye kuwa Rais wa nne wa Tanzania.
Historia inamtaja Lowassa kama mwanajeshi aliyehudumu katika Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), ambapo mnamo mwaka 1978, Lowassa alijiunga na jeshi la ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kwenda vitani wakati wa vita vya Kagera, kati ya Tanzania na Uganda vilivyodumu kwa miezi 6 na kumalizika April.1979.
Baadaye mwaka 1984 Lowassa alitunukiwa Shahada ya pili ya Maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Bath cha Uingereza.
Jina la Lowassa lilianza kufahamika zaidi kwa umma baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha kimataifa cha mikutano Arusha, (AICC) na baadaye kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa Uongozi wa Rais wa pili, Ali Hassan Mwinyi.
Mwaka 1995 Lowassa alitia nia kuwania kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais, lakini jina lake lilichujwa katika hatua za awali katika mchakato uliompa ushindi Hayati Benjamin Mkapa ndani ya chama na katika uchaguzi mkuu.
Mwaka huo huo 1995 Lowassa alishinda Ubunge wa Monduli kisha mwaka 1998 aliteuliwa na Rais Mkapa kuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Mkamu wa Rais akihusika na Mazingira na kupambana na Umaskini.
Mbali nafasi hiyo mwaka 2000 aliteuliwa kuwa Waziri wa Maji hivyo alihudumu katika nafasi hiyo na ilipofika Mwaka 2005 aliamua kumuunga mkono rafiki yake wa miaka mingi, Jakaya Kikwete katika kuwania kuteuliwa na CCM kuwania Urais dhidi ya wagombea wa upinzani.
Baada ya Kikwete kupata ushindi mkubwa wa zaidi ya asilimi 80, Lowassa aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa 9 wa Tanzania. Alijipatia sifa kubwa ya uchapakazi hususan katika ufuatiliaji wa utendaji serikalini.
Alivyojiuzulu nafasi yake ya Waziri Mkuu
Hata hivyo, Lowassa alidumu kwenye nafasi ya uwaziri mkuu kwa miaka miwili na mwezi mmoja hivi, tarehe 7 Februari 2008 alilazimika kujiuzulu kutokana kashfa ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, ambayo kupitia uchunguzi wa Kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na mbunge Dkt. Harrison Mwakyembe ilibainika kuwa ililipwa fedha nyingi licha ya utendaji duni uliolenga kuikwamua nchi kutoka kizani.
Hii ilikuwa baada ya ripoti ya Kamati ya uchunguzi ya Bunge kuwasilishwa bungeni, huku Lowassa akilalamika kabla ya kujiuzulu kuwa alikuwa ameonewa na kudhalilishwa sana kwa kutosikilizwa na Kamati hiyo ya Dkt. Makyembe.
Hoja ya kujiuzulu ilizidi kumpa umaarufu Lowassa, huku wengine wakimtathimini kama mwanasiasa aliyekomaa katika siasa, kwani suala la kujiuzulu kwa wanasiasa hasa wa Afrika ni gumu sana.
Alivyohamia na kuondoka CHADEMA
Mnamo Julai 25, 2015, Edward Lowassa, waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, alishtua ulimwengu wa siasa kwa kuondoka CCM na kujiunga na Chadema. Hilo lilitokea baada ya kutofaulu katika mchujo wa CCM na hivyo akaibukia katika kikao cha Kamati Kuu cha Chadema.
Lowassa alikaribishwa CHADEMA na ndipo hapo akaianza upya safari yake ya siasa katika chama cha upinzani, ambapo huko alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mgombea Urais kupitia muungano wa vyama vya upinzani maarufu kama UKAWA.
Tarehe 29 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva alimtangaza hayati Magufuli kuwa mshindi wa kiti cha Urais kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58 huku mpinzani wake wa karibu Edward Lowasa akipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39 nukta 97.
Hata hivyo pamoja na kushindwa kwenye kinyang’anyiro hicho Lowassa bado aliamini kuwa yeye ndiye mshindi wa kiti hicho isipokuwa alifanyiwa hujuma kutokana na wizi wa kura uliofanywa na Chama cha Mapinduzi CCM
Baada ya hekaheka za uchaguzi kuisha Lowassa aliendelea na mapambano ya siasa akiwa ndani ya CHADEMA, hata hivyo akabadili upepo na kuamua tena kurudi CCM
Machi 1, mwaka 2019 Lowassa aliachana na Chadema na kurejea CCM akipokewa na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wakati huo, hayati John Magufuli.
Tangu Machi 2023, afya ya Lowassa ilielezwa kuteteleka pale ilipotangazwa alikuwa amelazwa huspitalini nchini Afrika Kusini. Tangu wakati huo hapakuwepo taarifa za mara kwa mara juu ya hali ya afya yake hadi kutangazwa kifo chake.
Lowassa amefarikI Februari 10,2024 siku ya Jumamosi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko jijini Dar es salaam.
Akitangaza kifo cha kiongozi huyo, Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt Philip Mpango amesema Lowassa amefikwa na umauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete wakati wakipatiwa matibabu.
”Amefariki leo akipatiwa matibabu kwa ugonjwa wa kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu. Hayati Ngoiyai Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu tangu tarehe 14 mwezi Januari mwaka 2022”. Alisema Dkt. Mpango
Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu,” alisema makamu huyo wa rais.
Alikuwa akipatiwa matibabu katika taasisi hiyo ya moyo kisha kupelekwa Afrika Kusini na baadaye kurudishwa tena katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete.
Mwili wa Lowassa unatarajiwa kuzikwa Februari 17,2024 huko Monduli jijini Arusha ambako ndipo chimbuko la maisha yake.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza familia na mamia ya wananchi katika mazishi ya Lowassa.