Madeleka afunga ukurasa wa ACT Wazalendo, ageukia harakati za haki

Wakili na mwanaharakati wa haki za binadamu Peter Madeleka ametangaza rasmi kujiondoa ndani ya Chama cha ACT Wazalendo, akisema anataka kutumia muda na nguvu zake zaidi katika kupigania haki za wananchi na ustawi wa taifa nje ya siasa za chama.

Madeleka alitangaza uamuzi huo kupitia tamko alilolitoa jana Julai 26, 2026, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kumpa nafasi ya kushirikiana na watu wote wanaotetea haki bila kujali misimamo yao ya kisiasa.

“Leo tarehe 26 Julai 2026 mimi Peter Madeleka ninatangaza rasmi kuachana na siasa za ACT Wazalendo. Ninafanya hivyo ili nipate muda wa kutosha kuungana na wapenda haki wote katika kupigania haki na ustawi wa nchi yetu. Tanzania yenye haki inawezekana kama kila mtu atatimiza wajibu wake,” amesema katika tamko hilo.

Madeleka alijiunga na ACT Wazalendo mwaka 2025, hatua iliyotafsiriwa na wengi kama kuhamia moja kwa moja katika siasa za vyama baada ya miaka mingi kujijengea jina kama wakili na mtetezi wa haki za binadamu.

Katika kipindi chote cha taaluma yake, Madeleka amefahamika kwa kushughulikia kesi zinazohusu haki za msingi, uhuru wa kujieleza, pamoja na kuwawakilisha wanaharakati, waandishi wa habari na wanasiasa wa upinzani katika mashauri mbalimbali yaliyovuta hisia za umma.

Mbali na taaluma ya sheria, amekuwa mmoja wa sauti zinazojitokeza mara kwa mara kukosoa ukiukwaji wa haki za binadamu na kutoa maoni kuhusu umuhimu wa utawala wa sheria, uhuru wa mahakama na ulinzi wa Katiba.

Ingawa hakueleza sababu nyingine za ndani ya chama zilizomsukuma kuondoka ACT Wazalendo, msisitizo wake ulikuwa kwamba anataka kuwa sehemu ya juhudi pana za kutetea haki bila kufungamana na shughuli za chama cha siasa.