Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha katika kuhakikisha linakomesha matukio ya ajali kuelekea mwisho wa mwaka katika Mkoa huo limeendelea kutoa Elimu kwa madereva na kuwafungia leseni za udereva madereva watano (05) kwa makosa mbalimbali.
Akitoa taarifa hiyo leo Novermber 16 kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kamishna msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema kuwa madereva hao wamefungiwa leseni zao kwa muda wa miezi mitatu hadi sita kwa makosa mbalimbali ikiwemo ulevi, mwendokasi, kusababisha ajali, wenye makosa yanayojirudiarudia pamoja na wale ambao wanayapita magari mengine (overtaking) sehemu ambazo zimekatazwa kisheria.
Kamanda Masejo amebainisha kuwa Jeshi hilo limefanikiwa kutoa elimu katika nyumba za ibada, stendi za mabasi, mashuleni, vijiwe vya bodaboda pamoja na masoko ambapo jamii hiyo imepata uelewa wa kutosha kuhusiana na sheria mbalimbali za usalama barabarani.
Aidha ACP Masejo ametoa onyo kali kwa madereva wanaoendelea kuvunja sheria za usalama barabarani kuwa Jeshi hilo halito muonea muhali dereva yeyote kwa makosa ya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani.Pia amewaomba wananchi kutoa taarifa za uhalifu na walifu ili kuuufanya Mkoa huo kuwa shwari.