Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, Wakili Gaston Garubindi, maombi hayo yamesajiliwa na kupangwa mbele ya Jaji Obadia Bwegoge.
Mahakama Kuu ya Tanzania, masijala ndogo ya Dar es Salaam, imepokea rasmi maombi ya Habeas Corpus(amri ya kumtaka mtuhumiwa afikishwe mahakamani kuthibitisha uhalali wa kizuizi chake) kwa ajili ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, ambaye amekuwa kizuizini tangu Oktoba 22, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA, Wakili Gaston Garubindi, maombi hayo yamesajiliwa na kupangwa mbele ya Jaji Obadia Bwegoge.
“Tunafuatilia wito wa mahakama (summons) kwa wajibu wa maombi ambao ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na wenzake watano,” amesema Garubindi kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Alhamisi, Novemba 6, 2025.
Garubindi amesema maombi hayo yamewasilishwa baada ya maombi ya awali yaliyotumika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kukumbwa na changamoto za kiufundi za mtandao, wakati ambapo Heche alihamishwa kutoka Dodoma kurejeshwa Dar es Salaam.
Heche alikamatwa tarehe 22 Oktoba 2025, na awali ilidaiwa kuwa alisafirishwa kuelekea Tarime. Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa alishikiliwa Kituo cha Polisi Mtumba, jijini Dodoma, bila kufikishwa mahakamani au kupewa dhamana kwa mujibu wa sheria.
“Baada ya jitihada za ufuatiliaji na msaada wa wasamaria wema, tulibaini kuwa alikuwa akishikiliwa Mtumba. Juzi alisafirishwa tena hadi Dar es Salaam, ambako alifika jioni,” imeeleza taarifa hiyo.
CHADEMA imesema itaendelea kuwajulisha wananchi kuhusu mwenendo wa maombi hayo ya Habeas Corpus, ambayo kimsingi yanataka mahakama iamuru mamlaka za polisi kumfikisha Heche mahakamani ili kubaini uhalali wa kizuizi chake.
Itakumbukwa kuwa Heche awali alipofikishwa Polisi Dar es Salaam na baadae kusafirishwa hadi jijini Dodoma alikua anakabiliwa na shtaka la kuvuka mpaka wa Tanzania kwenda nchini Kenya kinyume na sheria, hata hivyo sasa anakabiliwa na mashtaka mawili ya Ugaidi ambayo kwa mujibu wa Polisi anadaiwa kuyafanya hivi karibuni kwa kuchochea vurugu wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni.