Mahakama Kuu ya Marekani kusikiliza kesi dhidi ya vitabu vya LGBTQ Mashuleni

Mahakama Kuu ya Marekani, ambayo ina wingi wa majaji wa mrengo wa kihafidhina, inatarajiwa kusikiliza kesi leo Jumanne kuhusu iwapo wazazi wana haki ya kidini kuwazuia watoto wao kuhudhuria madarasa yanayosoma au kujadili vitabu vyenye maudhui ya LGBTQ.

Mahakama hiyo itapitia rufaa iliyowasilishwa na wazazi dhidi ya wilaya ya shule za umma katika jimbo la Maryland, ambako mnamo mwaka 2022, vitabu vilivyo na lengo la kupambana na chuki na kujadili masuala ya ushoga na utambulisho wa kijinsia vilijumuishwa katika mitaala ya wanafunzi wa chekechea na shule za msingi.

Awali, shule hizo ziliwaruhusu wazazi kuwatoa watoto wao kwenye masomo hayo yenye utata, lakini baadaye walifuta ruhusa hiyo, wakisema: “Utaratibu huo wa kuwatoa watoto ulikuwa mgumu kutekelezeka. Baadhi ya shule, kwa mfano, zilishuhudia idadi kubwa ya wanafunzi wasiohudhuria masomo.”

Wazazi sasa wamefungua kesi wakidai kufutwa kwa ruhusa hiyo kunakiuka imani zao za Kikristo na Kiislamu, pamoja na haki zao za Kikatiba chini ya Marekebisho ya Kwanza (First Amendment). 

Malalamiko yao yanaeleza kuwa bodi ya shule ya Kaunti ya Montgomery “inalenga kuvuruga” haki za wazazi kulea watoto wao katika misingi ya imani zao.

Katika baadhi ya majimbo yenye mwelekeo wa kihafidhina, mifumo ya shule tayari imeanza kupiga marufuku baadhi ya vitabu au kuondoa machapisho fulani kwenye maktaba, huku wazazi na makundi ya kihafidhina wakisema kuwa si sahihi kwa maeneo ya umma kuwa na vitabu vinavyoshabikia ushoga na mitazamo jumuishi ya kisasa.

Gavana wa Florida, Ron DeSantis, kutoka chama cha Republican, mnamo mwaka 2022 alisaini sheria inayojulikana sana kama “Don’t Say Gay”, inayopiga marufuku ufundishaji wa mada zinazohusu mwelekeo wa kingono au utambulisho wa kijinsia katika shule za msingi.

Kulingana na hukumu zilizotolewa hapo awali na mahakama, kuwafundisha wanafunzi mawazo yanayokwenda kinyume na dini yao hakuhesabiwi kama kulazimisha imani.

Idara ya Haki ya serikali ya Rais wa zamani Donald Trump inaunga mkono wazazi katika kesi hiyo, ikizishtumu shule kwa kile ilichokiita “kuingilia waziwazi uhuru wa kuabudu.”

Uamuzi wa Mahakama Kuu, ambayo ina majaji sita wa kihafidhina na watatu wa mrengo wa kisasa, unatarajiwa kutolewa kabla ya mwisho wa kikao cha sasa mnamo mwisho wa mwezi Juni.