Mahakama Kuu nchini Tanzania kanda ya Dar es salaam imesema uamuzi wa kumwondoa katika utumishi wa umma aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nchini humo, Profesa Mussa Assad ulikiuka Katiba.
Uamuzi huo ulitolewa jana Jumatatu Desemba 5, 2022 na jopo la majaji watatu, Dk Benhajj Masoud (kiongozi wa jopo), Juliana Masabo na Edwin Kakolaki kufuatia kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.
Profesa Assad aliteuliwa kushika wadhifa huo na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Novemba 5, 2014 na alihudumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitano hadi Novemba 4, 2019 baada ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli kutengua uteuzi wake na kumteua CAG wa sasa Charles Kichere kushika wadhifa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali ya Tanzania mwaka 2019 ilieleza kuwa Profesa Assad kipindi chake kilimalizika Novemba 4, 2019.
Zitto aliamua kufungua kesi ya Kikatiba mahakamani hapo akipinga kuondolewa kwa Profesa Assad katika wadhifa huo na uteuzi wa Kichere kuwa CAG mpya, akidai kuwa Profesa Assad alikuwa hajatimiza muda wake wa utumishi kikatiba yaani umri wa kustaafu.
Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 8 ya mwaka 2020, Zitto akiwakilishwa na mawakili Dk Rugemeleza Nshala na Nyaronyo Kichere, alikuwa akipinga kuondolewa kwa Profesa Assad na kuteuliwa kwa Kichere kuwa ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Alidai kuwa kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma namba 11 ya mwaka 2008 kinachoweka mihula miwili ya miaka mitano ya utumishi wa CAG, ambacho ndicho kilichotumika kuondolewa kwa Profesa Assad, kinakinzana na masharti ya Katiba.
Zitto alidai kuwa Ibara ya 144(1) ya Katiba ambayo inaeleza kuwa CAG atatumikia wadhifa huo mpaka umri wake wa kustaafu, yaani miaka 60 kikatiba au miaka 65 kisheria, sawa na kifungu 62(a) cha sheria hiyo kinavyoeleza.
Hivyo, alikuwa akiiomba mahakama hiyo itamke kuwa kifungu hicho cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi, ni batili kwa kuwa kinakinzana na Katiba na kwamba kuondolewa kwa Profesa Assad kabla ya kutimiza umri wa kustaafu ni batili na pia uteuzi wa Kichere kuwa CAG mpya ni batili.
Mahakama hiyo katika hukumu yake iliyosomwa jana ilikubaliana na hoja za Zitto kuwa kifungu hicho cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi kuweka mihula ya miaka mitano mitano ya utumishi wa CAG ni batili kwa kuwa kinakinzana na Katiba Ibara hiyo ya 44 ambacho kinaendana na Katiba.
Mahakama hiyo imesema kuwa wakati kifungu hicho kinaweka mihula ya utumishi wa CAG, Katiba inazungumzia umri wa kustaafu na si mihula.
Hivyo, Mahakama imesema kuondolewa kwa Profesa Assad kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kulikuwa ni batili.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imekataa maombi ya Zitto kutamka kuwa uteuzi wa Kichere ni batili, badala yake imesema kuwa uteuzi wake ni halali kwa kuwa aliteuliwa kwa mujibu wa Katiba.
Wakili Nshala amesema pamoja na Mahakama kutamka hivyo lakini imeacha utata baada ya kukubali kuwa kuifungu hicho cha sheria kinachoweka mihula badala ya umri ni batili na kwamba Profesa Assad aliondolewa kinyume cha Katiba lakini ikasema kuwa uteuzi wa Kichere ni halali.
Zitto katika taarifa yake kwa umma akizungumzia kipengele hicho amesema kuwa amewaelekeza mawakili wake kukata rufaa Mahakama ya Rufani kwa lengo la kubatilisha uteuzi wa Kichere.
“Hata hivyo, Mahakama imekataa kukubali maombi yetu kuteuliwa CAG mwingine ilikuwa batili. Hili tutakwenda Mahakama ya Rufaa ili iweze kulitolea maamuzi. Kama kuondolewa kwa Prof. Assad ilikuwa batili ni dhahiri kuwa kuteuliwa kwa mtu mwingine kushika nafasi hiyo ilikuwa batili pia. Nimeshatoa maelekezo kwa mawakili wangu wakate Rufaa katika eneo hilo la hukumu.”
Wakili Nshala alisema kuwa wako tayari kwa maelekezo ya mteja wao, Zitto kukata rufaa Mahakama ya Rufani katika kipengele hicho ili kupata ufafanuzi zaidi.