Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam imetengua hukumu iliyotolewa na mahakama ya wilaya ya ilala dhidi ya mfanyabiashara Zarina Mohamed Sadiki aliyehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kumtukana mama yake mzazi
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Juliana Masabo wa mahakama hiyo, ambaye alisema mrufani (Zarina) alikuwa na hoja saba za kupinga hukumu hiyo iliyomtia hatiani ikiwa ya Mahakama ya Ilala kukosea kumtia hatiani na kumfunga mrufani kwa kuwa mashtaka dhidi yake hayakuthibitishwa pasipo kuacha shaka na upande wa mashtaka.
Alisema mahakama hiyo pia ilikosea kumtia hatiani Zarina na kumfunga kwa sababu kulikuwa hakuna ushahidi uliotolewa dhidi yake na mahakama hiyo haikuchambua ipasavyo ushahidi, kwa kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka haukuwa na uhakika.
Pia Jaji Masabo alisema ushahidi wa mrufani haukuzingatiwa na ushahidi wa mashtaka ulikuwa wa kusikia na sio wa kuungana jumuishi.
Jaji Masabo alisema mrufani alidai kuwa mashtaka dhidi yake hayajulikani, kwamba alitoa lugha ya matusi dhidi ya mama yake Novemba 29, 2019 haikufafanua muda gani alitoa lugha hiyo.
“Ingawa inadaiwa kuwa mrufani alito lugha hiyo ya matusi mbele ya mteja wake, lakini mteja wake hakuja kutoa ushahidi mahakamani,” alisema Jaji Masabo na kuongeza:
“Kutokuitwa kwa shahidi huyo ambaye alikuwa ni shahidi wa muhimu katika kesi hiyo, kunafanya mashtaka dhidi mrufani kutothibitika.”
Jaji Masabo alisema wakati Wakili wa Zarina anatoa hoja zake, alieleza kuwa mahakama haikutambua kama maneno yaliyozungumzwa yalikuwa ni matusi au la.
Aliendelea kufafanua kuwa dukani hapo kulikuwa na CCTV kamera, ilitarajiwa upande wa mashtaka ungewasilisha ushahidi huo, lakini haukufanyika hivyo.
Jaji Masabo alisema: “Mahakama baada ya kusikiliza hoja pande zote mbili, nakukubaliana na wakili wa mrufani kwamba kesi dhidi yake haijathibitishwa, hivyo hatia na kifungo dhidi ya mshtakiwa imeondolewa na imeamriwa ya kwamba aachiwe labda kama anashtakiwa na kesi nyingine kisheria.”
Hukumu hiyo ya Mahakama ya Ilala ilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Martha Mpaze, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mashtaka ukiwamo ushahidi wa mama yake mzazi, Rafika Hawa Sidik.