Search
Close this search box.
Africa

Mahakama yapanga kusikiliza rufaa ya Sabaya siku tano mfululizo

15

Rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kupinga hukumu iliyomwachia huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake, imepangwa kuendelea kusikilizwa kwa siku tano mfululizo kuanzia Februari 27, 2023.

Rufaa hiyo namba 155/2022 mbali na Sabaya wajibu rufaa wengine ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Akiahirisha rufaa hiyo leo Jumanne, Januari 17, 2023, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Judith Kamala amesema rufaa hiyo itasikilizwa mfululizo kuanzia Februari 27 hadi Machi 3, 2023 na Jaji Salma Maghimbi.

Leo muomba rufaa amewakilishwa na Wakili wa Serikali, Alice Mtenga huku Sabaya akiwakilishwa na wakili Mosses Mahuna, mjibu rufaa wa pili Mnkeni ambaye pia alikuwepo mahakamani hapo akiwakilishwa na wakili Sabato Ngogo huku Aweyo na Nyegu ambao hawakuwepo mahakamani hapo wakiwakilishwa na wakili Fridolin Bwemelo.

Awali rufaa hiyo iliyoahirishwa mara ya mwisho Jamuari 9, 2023 ilielezwa mahakamani hapo kuwa itaendelea kusikilizwa leo, Januari 17.

Rufaa hiyo inasikilizwa na Jaji Salma Maghimbi ambaye Desemba 14, 2022 aliahirisha rufaa hiyo na kutoa amri kwa Naibu Msajili huyo, kuchapisha kwenye magazeti tangazo la hati ya wito kwa wajibu rufaa wanne kwenye rufaa hiyo ambao hawakuwepo mahakamani hapo ambao ni Mnkeni, Aweyo, Macha na Msuya.

Wakili Mahuna aliieleza mahakama licha ya matangazo hayo kutolewa kwenye magazeti hadi sasa wajibu rufaa wawili ambao ni Macha na Msuya hawajafika mahakamani hapo.

Rufaa hiyo dhidi ya Sabaya na wenzake watano inapinga hukumu iliyotolewa Juni 10, 2022  na Hakimu Mkazi Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, hukumu iliyowaachia Sabaya na wenzake sita waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi  namba 27/2021 katika mahakama hiyo ya chini.

Comments are closed

Related Posts