Maelfu ya raia wa Ukraine wanajaribu kuukimbia mji wa Mariupol wakati Urusi ikiendeleza mashambulizi ya mabomu kwenye mji huo wa bandari.
Kulingana na Shirika la Human Rights Watch, watu waliofanikiwa kuukimbia mji huo wameelezea hali mbaya walioiacha ikiwemo maiti kutapakaa barabarani na majengo yaliyoharibiwa.
Katika ujumbe wake kwa njia ya video, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kundi la watu waliokuwa wakikimbia mapigano hayo kwa kutumia njia salama zilizokubalika wamekamatwa na wanajeshi wa Urusi.
Ameongeza kwamba, kuna takriban watu 100,000 katika mji huo wanaoishi katika mazingira magumu na wanakosa huduma za msingi ikiwemo chakula, maji, dawa na umeme.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine amesema tangu kuanza kwa vita hivyo mnamo Februari 24, watoto wapatao 117 wameuawa huku shule 548 zikiharibiwa.
Wakati hayo yakiendelea Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ameitolea mwito Urusi kumaliza vita hivyo. Guterres amesema vita hivyo havina maana.