Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameliomba bunge kuidhinisha shilingi bilioni 148.9 kwa ajili ya matumizi ya Ofisi yake na taasisi zake kwa mwaka 2022/23, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 101.36 zikienda kwenye matumizi ya kawaida na zaidi ya shilingi bilioni 47.5 zikienda kwenye miradi ya maendeleo.
Waziri Mkuu ameomba fedha hizo leo kwenye hotuba ya Maombi ya Makadilio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2022/23 katika mkutano wa bunge Jijini Dodoma.
Aidha ameomba kuidhinishiwa zaidi ya shilingi bilioni 132.7 kwa ajili ya mfuko wa bunge kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 127.3 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya maendeleo.
Katika hotuba yake Waziri Majaliwa amezungumzia upandaji wa bidhaa akisema Serikali imeagiza tume ya ushindani kufuatilia taarifa za uhaba na upandaji wa bei usioendana na uhalisia.
Amesema Serikali imezingatia katika upandishaji wa bidhaa kwa kutumia sheria namba 8 ya 2003 ambayo inazuia kupanda kwa bidhaa kwa ajili ya kusaidia wananchi kupunguza makali ya maisha ikiwemo kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Nawasihi wazalishaji na wafanyabiashara kuuza bidhaa kwa bei zinazotakiwa na pale itakapobidi kwa watakaopandisha bei ya bidhaa muhimu pasipokuendana na bei halisi, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,” amesema Waziri Mkuu
Hata hivyo amesema katika mwaka 2021, mfumuko wa bei ulikua kwa wastani wa asilimia 3.7 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2020.
Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kulichangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo atahari za Uviko-19, kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma, kupungua kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya masoko ya ndani kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa mfumuko huo ulikuwa ndani ya lengo la muda wa kati ya asilimia 3 – 5 ambapo wigo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki usiozidi asilimia 8 na ndani ya wigo 17 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika wa kati ya asilimia 3 – 7.