Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema asilimia 23 ya nyongeza ya mishahara iliyotamkwa iliwalenga watumishi waliokuwa wanalipwa kima cha chini ambao ni kati ya asilimia 75 hadi 78 ya wafanyakazi wote.
Majaliwa ametoa ufafanuzi huo leo Ijumaa Julai 29, 2022 wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu nyongeza ya mishahara, ikiwa ni siku chache baada ya watumishi kulalamikia nyongeza hiyo na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kupinga.
Miongoni mwa malalamiko ya watumishi, ni kiwango kidogo cha nyongeza ya mishahara hiyo, ambayo Majaliwa amesema si wafanyakazi wote walioongezewa kwa asilimia 23, bali ni wale waliokuwa wanalipwa kima cha chini.
“Inapotamkwa wanaonufaika si wote hadi wa mishahara mikubwa, wanaonufaika ni wale wa kada ya chini, ambao kwa tangazo la mwaka huu wanufaika ni asilimia 75 hadi 78 ya watumishi wote,” amesema.
Amefafanua kuwa asilimia za nyongeza ya mishahara inapungua kwa kadri ya ukubwa wa kiwango cha malipo anachopata mfanyakazi, akitolea mfano mawaziri wameongezewa asilimia 0.7.
“Sasa ile asilimia inayotamkwa inawalenga wale wenye kima cha chini sio tu wale walioanza kazi hata wale waliotangulia lakini, wapo kwenye kima cha chini kwa lengo la kuinua kipato chao ili wapate kiwango kitakachokidhi mahitaji haya kutokana na mabadiliko ya uchumi nchini,” amesema.
Watumishi wenye mishahara mikubwa, amesisitiza kuwa hawaongezewi asilimia 23 kama ilivyotamkwa, bali nyongeza yao inafanyika kulingana na fomula za viwango vya malipo vilivyopo.
“Kuna fomula ya malipo ambayo asilimia inapungua ili kuwaweka watu katika mfumo usioleta pengo kubwa kutoka mmoja kwenda mwingine,” amesema.
Hata hivyo, Majaliwa amesema licha ya asilimia hiyo ya nyongeza kutokidhi, lakini Serikali imeonyesha dhamira na hivyo makubwa zaidi yanatarajiwa kufanyika siku za usoni
Amebainisha nyongeza ya mishahara inafanywa kwa kuzingatia hali ya uchumi wa nchi.