Majambazi watatu waua mkoani Kagera.

Jeshi la Polisi mkoani Kagera limesema limewaua watu watatu wanaodhaniwa kuwa majambazi katika mpaka wa Wilaya ya Ngara na Biharamulo mkoani Kagera.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, ACP William Mwampagale amewaambia waandishi wa habari tukio hilo lilifanyika wakati wa operashani maalumu baada ya kupata taarifa kuwa kuna kundi lililokuwa linapanga kufanya uhalifu.

“Tulipata taarifa za kiintelijensia kuwa kuna kikundi cha majambazi kimepanga kufanya uhalifu kwa kutumia silaha Novemba 15, 2022. Tuliweka mitego katika maeneo hayo ambapo baada ya kuwanasa nakuanza majibizano ya risasi walijeruhiwa na kukimbizwa hospitali ambapo walipoteza maisha,” amesema.

Kamanda Mwampagale amesema miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Ngara Nyamiaga.

Amesema majambazi hao walikuwa watano wote wanaume waliokuwa wanakadiliwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 35 na katika uchunguzi wa awali uliofanywa na jeshi hilo umebaini kuwa kikundi  hicho kimekuwa kikifanya matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha tangu Septemba mwaka huu katika maeneo ya kijiji cha Bugarama,Muganza na Murusagamba.

Hata hivyo Mwampagale ameongeza kwa katika operashani hiyo wamefanikiwa kupata silaha moja aina ya AK47 isiyokuwa na namba pamoja na magazine moja ikiwa na risasi 12 na hivyo kutumia nafasi hiyo kuwaonya wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.