Majimbo mapya ya Uchaguzi yaliyotangazwa na INEC

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanzishwa kwa majimbo mapya nane ya uchaguzi pamoja na kubadilishwa kwa majina ya majimbo mengine 12, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo,Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, amesema uamuzi huo umezingatia ongezeko la watu, ukubwa wa maeneo ya kiutawala, pamoja na mahitaji ya uwakilishi wa karibu zaidi kati ya wananchi na wawakilishi wao bungeni.

Kwa mujibu wa Jaji Mwambengele, majimbo mapya yaliyoundwa ni kama ifuatavyo:

Dar es Salaam imegwanywa majimbo mapya ambayo ni Jimbo la Ukonga limegawanywa na kuanzishwa Jimbo la Kivule na Jimbo la Mbagala limegawanywa na kuanzishwa Jimbo la Chamazi.

Mbeya imegawanywa  Jimbo la Mbeya Mjini limegawanywa na kuundwa Jimbo la Uyole.

Dodoma mgawanyo wake umewekwa  Jimbo la Dodoma Mjini ambalo limegawanywa na kuundwa Jimbo la Mtumba.

Simiyu, Jimbo la Bariadi limegawanywa na kuundwa Jimbo la Bariadi Mjini.

Geita, Jimbo la Busanda limegawanywa na kuanzishwa Jimbo la Katoro na Jimbo la Chato limegawanywa na kuundwa Jimbo la Chato Kusini.

Shinyanga, Jimbo la Solwa limegawanywa na kuanzishwa Jimbo la Itwangi.

Aidha, Tume hiyo imesema majina ya majimbo 12 ya uchaguzi yatafanyiwa mabadiliko ili kuendana na mabadiliko ya kiutawala, kijografia na mahitaji ya kitaifa ya utawala bora. Orodha kamili ya majimbo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya majina inatarajiwa kutangazwa rasmi katika tangazo la serikali litakalotolewa hivi karibuni.

Tume imewahakikishia Watanzania kuwa mchakato huo umezingatia misingi ya usawa, haki na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali, na unalenga kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia uwakilishi wa kweli wa wananchi.

Ikumbukwe kuwa mgawanyo wa majibo haya unafaya kuongezeka kwa majimbo na kuwa 272 kutokana na ongezeko la majimbo mapya manane yaliyotangazwa leo ambapo 222 yakiwa Tanzania Bara huku 50 yakiwa Tanzania Zanzibar.