Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema kuwa magao wa umeme mkubwa na mkali waliokuwa wanatarajia ungekuwepo, hautakuwepo tena.
Amesema hayo akitoa taarifa ya serikali bungeni leo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina aliyehoji kuhusu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kukata kata umeme mara kwa mara.
“Nitoe kauli ya serikali kwamba, ule mgao tuliokuwa tunautarajia utakuwepo kwa makali yale na ukubwa ule, hautakuwepo,” amesema Byabato.
Ameeleza zaidi kwamba kukatika kwa umeme kunasababishwa na kuzidiwa kwa matumizi pindi wateja wote wanapowasha mitambo yao, na wakati matengenezo yanafanyika, mitambo ya wateja inakuwa imezimwa, hivyo matengenezo yanapokamilika, wateja wakiwasha mitambo, umeme unakatika tena.
Kuhusu suala la mgao wa umeme ameeleza kuwa hautakuwa mkubwa kama walivyotarajia baada ya hatua kadhaa kuchukuliwa kuupunguza ambapo amezitaja hatua hizo kuwa ni
- Wamebaini kwamba wanaweza kupitisha kiasi cha gesi kwenye mitambo ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), na hivyo kufidia upungufu wa gesi ambayo ungetokea kutokana na matangenezo ya mitambo ya PAET.
- Kwa sasa mabwawa ya kufua umeme yameanza kurudi katika hali nzuri na hivyo yataweza kuongeza kiwango cha uzalishaji na kusaidia maeneo ambayo yalikuwa yakose umeme.
- Walitarajia kwamba kungekuwa na uhitaji mkubwa sana wa umeme, lakini baada ya kufanya uchunguzi wamebaini kwamba kile walichodhani kitahitajika, sicho kinachohitajika. Ameeleza kwamba awali walidhani watahitaji takribani megawati 300, lakini uhalisia unaohitajika ni megawati 100
Amesema katika kipindi cha mgao mdogo wa umeme, watatumia nafasi hiyo kufanya marekebisho ikiwemo kupunguza umeme kwenye njia zilizozidiwa, kukata miti ambayo imekuwa ikiangukia nguzo, na kuboresha vituo vya kupoza umeme.